Wakulima Morogoro washauriwa kujiunga katika vyama vya ushirika

Serikali mkoani Morogoro imewasisitiza wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika Ili kunufaika na sekta hiyo ikiwemo kuuza bei nzuri ya Mazao yao pamoja na vipimo sahihi vya mizani.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebecca Nsemwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima katika Jukwa la nne la maendeleo vyama vya ushirika lililofanyika Mkoani humo ambapo amesema kuwa ushirika umekuwa Mkombozi Kwa wakulima hasa vijijini

Anasema kumekua na malalamiko mengi ya Wakulima kuhusu kupunjwa bei ya kuuza Mazao pamoja na vipimo hivyo kupitia ushirika kila mkulima ananufaika kupitia sekta hiyo kwa kuuza stakabadhi gharani.


Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Keneth Shemdoe, amesema uwepo wa changamoto za migogoro, kesi, utendaji usio ridhisha wa viongozi pamoja na baadhi ya watendaji na wajumbe wa bodi kuwa na uelewa unachangia kutofikiwa malengo ya vyama hivyo.

Amesema bado vyama hivyo vimekuwa vikitumia mifumo ya kizamani katika utunzaji wa kumbukumbu hali ambayo huchangia kukosekana kwa taarifa na Takwimu kwenye vyama pindi zinapohitajika huku kukosekana kwa ubunifu wa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kutokuajiri watendaji wenye sifa kunavyo zorotesha utendaji wa vyama vya ushirika.

Aidha amesema licha ya vyama hivyo kukakabiliwa na changamoto hizo katika mikakati yake, vimekusudia kusajili vyama vipya vya ushirika kulingana na mahitaji ya kiuchumi ya wananchi, kufufua vyama vya msingi vya ushirika ambavyo havifanyi kazi ipasavyo, kuendelea kuhamasisha vyama vya ushitika kuajiri watendaji wenye sifa, kuendelea kusimamia majukwaa ya maendeleo ya ushirika pamoja na kusimamia mfumo wa stakabadhi za ghala kwa kila Halmashauri za Mkoa wa Morogoro.

 

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Morogoro Iddi Bilali alisema wamefanikiwa kuanzisha mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika kwa ajili ya kuendesha shughuli za ushirika kidigitali, ambapo jumla ya vyama 212 vimesajiliwa kwenye mfumo huo, vyama 21 vikinufaika na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku, vyama 38 vya akiba na mikopo vimepata leseni ya Benki Kuu na wanachama na viongozi wa Vyama 86 wamepatiwa elimu ya uendeshaji wa shughuli za vyama.

Amesema wamefanikiwa pia kusimamia uuzaji wa baadhi ya mazao ya kimkakati kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani za Halmashauri za Mkoa wa Morogoro ambapo kwa zao la Kakao jumla ya minada 56 imefanyika, kilo 3,210, 355 zimeuzwa kwa thamani ya Tsh 33,748,289,930.00

Related Posts