MZUMBE, TAMONGSCO WAPONGEZWA KWA KUTOA MAFUNZO KWA WAMILIKI WA SHULE NA VYUO

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

WAMILIKI na Mameneja wa shule na Vyuo vya kati visivyo vya serikali nchini wamekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na Shirikikisho la Wamiliki wa shule na vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO) kwa kuwaandalia mafunzo ya namna ya uendeshaji wa shule na vyuo.

Pia wamepongeza kupatiwa fursa ya kutoa maoni juu ya sera na sheria ya elimu ya mwaka 1978 ili kamati inayohusika na ukusanyaji wa maoni, kuchukua maoni yao na kuona sheria inaweza kuboreshwa au kubadilishwa.

Akizungumza na waandishi leo Desemba 17,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ndaki ya Chuo hicho, Mshiriki wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Meneja wa Shule ya The Glory iliyopo Mafinga, Mathew Alex amesema Serikali inatakiwa kuwashirikisha walimu waliopo katika shule binafsi  kuanzia kwenye utungaji wa mitihani, usimamizi wa mitihani na semina mbalimbali.

Amesema masuala ya ushirika na ubia kati ya Serikali na wadau binafsi, wanaomiliki shule binafsi watazamwe kama ni kitu kimoja chenye kutoa huduma kwa jamii sio kama vitu viwili tofauti.

“Utoaji wa elimu katika shule binafsi ni huduma, sio biashara kama ambavyo wengi wanaielezea”. Amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wamiliki wa Shule na Vyuo binafsi nchini (TAMONGSCO), Alfred Luvanda amesema kuwa sheria ya elimu iliyopo inatazama zamani hivyo kuna umuhimu ikaboreshwa, vitu ambavyo havikuwepo vinatakiwa kuongezwa ili mifumo ya elimu iweze kufanya kazi.

“Tunashukuru tumetembelewa na kamati ya ukusanyaji wa maoni kwaajili ya maboresho ya sheria ya mwaka 1978, tunaupeo mpana hivyo watatusikiliza na kuchukua maoni yetu”. Amesema

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kukusanya Maoni kwaajili ya Mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, Prof. Saudin Mwakaje amesema Wamiliki wa shule na Vyuo binafsi ni mojawapo ya wadau muhimu katika utoaji wa elimu nchini, hivyo basi wameona kuna umuhimu mkubwa wa kukusanya maoni yao kwao.

“Kwenye kikao cha leo tutawapa licha nzima ya ile kazi ambayo inafanywa na kamati yetu kisha tutawakaribisha nao watueleze maoni yao, kwasababu wamekabili changamoto nyingi ambazo inapaswa ziboreshwa katika sheria ya elimu”. Amesema Prof. Mwakaje.

Vilevile kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya msingi Consolatha Lupembe iliyopo mkoani Njombe, Gisela Masika amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka wakati tunapolekea kwenye mabadiliko ya sera na sheria ya elimu ya mwaka 1978.

Related Posts