Bashe aingilia kati bei ya mbegu

Dodoma. Waziri wa Kilimo,  Hussein Bashe ametoa saa 24 kwa wazalishaji wa mbegu nchini kuwasilisha gharama za uzalishaji wa mbegu kwenye Taasisi ya uthibiti wa ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) na atakayekaidi agizo hilo atafutiwa kibali cha kuzalisha mbegu.

 Aidha amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TOSCI, Patrick Ngwediagi kuhakikisha wazalishaji hao wa mbegu wanafanya hivyo vinginevyo atapoteza nafasi yake.

Bashe ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Desemba 17, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na wazalishaji wa mbegu na mbolea nchini, kuhusu mfumo wa kuuza mbegu kwa ruzuku kwa wakulima.

Amesema kitendo cha wazalishaji hao kutopeleka gharama za uzalishaji wa mbegu Tosci imesababisha kununua mbegu kwa gharama kubwa ambayo hawawezi kuimudu.

“Wangapi ambao wamepeleka gharama za uzalishaji wa mbegu Tosci? (akasimama mtu mmoja) sasa nawaagiza kila mzalishaji wa mbegu apeleke gharama za uzalishaji wa mbegu Tosci ndani ya saa 24 na atakayekiuka nafuta leseni yake, na wewe Mkurugenzi kama hutaniletea hizo gharama hutakuwa na kazi,” amesema Bashe.

Amesema Tosci kutojua gharama halisi za uzalishaji wa mbegu zinasababisha wafanyabiashara kuwauzia mbegu wakulima kwa bei kubwa, kwani kuna maeneo ambayo mbegu ya mahindi kilo mbili inauzwa Sh25,000.

“Nilikuta Ruvuma kilo mbili za mahindi zinauzwa Sh25,000 namuuliza Agro dealer ananiambia amenunua mbegu hizo kwa Sh20,000 kwa hiyo ameweka na gharama zake za usafiri… nataka niwaambie kama mpaka siku ya Ijumaa saa nne asubuhi hujawasilisha gharama zako za uzalishaji tafuta biashara nyingine ya kufanya,” amesema Bashe.

Amesema Serikali ni lazima ijue gharama za uzalishaji ili ione bei itakayomsaidia mkulima badala ya kumkandamiza.

 Aidha amewataka wakulima hao kuuza mbegu zao kwa mfumo wa kidijitali ili kukomesha wauzaji wa mbegu bandia,  ambazo wamefanikiwa kuzikamata hivi karibuni.

Amesema mfumo wa kuuza mbolea kwa ruzuku umefanikisha kukomesha mbolea bandia ambazo zilikuwa zinasambazwa kwa wakulima na kuwasababishia hasara.

“Lakini kama kila kitu kitauzwa kwenye mfumo tutajua wazalishaji wa mbegu na mbolea bandia na tutawachukulia hatua za kisheria.

Katika kikao hicho wakulima wamelalamikia mfumo wa kidijitali wa kuuza mbegu kwa ruzuku kwa kuwa wakulima wengi hawajasajiliwa kwenye mfumo, hivyo waliiomba Serikali iruhusu na biashara ya pembejeo nje ya mfumo.

Anastazia Bwire ameiomba Serikali kuweka bei elekezi ya mbegu kwenye mfumo kama ilivyo kwenye bidhaa za mafuta, kwa kufanya hivyo mkulima akiuziwa mbegu kwa bei ambayo siyo elekezi atatoa taarifa na muuzaji atachukuliwa hatua za kisheria.

Ngwediagi amesema mpaka sasa jumla ya wakulima 4.14 milioni wameshaandikishwa kwenye mfumo na hakuna mkulima nchini ambaye atanunua pembejeo nje ya mfumo.

Aidha amesema pia idadi ya mawakala wa kilimo wameongezeka kutoka 1,703 mwaka 2023 hadi kufikia 2,877.

Related Posts

en English sw Swahili