Kibaha. Watu watano wakiwemo raia wa kigeni wamefikishwa mahakamani mkoani Pwani wakikabiliwa na mashItaka ya kuhujumu miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh200 milioni.
Waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha leo Desemba 17, 2024 ni Zhang Feng, Wang Yong, Paulo John, Abdul Mohamed na Pius Kitulya, wakazi wa Miwaleni, Mlandizi, wilayani Kibaha.
Mwendesha mashitaka Wakili wa Serikali, Joseph Kisaka amedai mahakamani hapo kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Novemba na Desemba, 2024.
Hakimu Felister Ng’welu anayesikiliza kesi hiyo amewataka washtakiwa kutojibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Baada ya kusomewa mashitaka wamepelekwa rumande. Kesi imepangwa kutajwa Desemba 30, 2024.
Kesi hiyo imevuta watu wengi waliofika mahakamani kuisikiliza.
Licha ya kusikilizwa jioni, baadhi ya watu waliokuwa nje ya mahakama baada ya kesi kuitwa waliingia ndani kusikiliza.