Dar es Salaam. Kesi ya mauaji inayomkabili mama anayedaiwa kumuua binti yake akishirikiana na kijana wake wa kiume imerejeshwa Mahakama Kuu ipangiwe jaji wa kuisikiliza.
Awali ilipangwa kusikilizwa na hakimu mkazi mwenye mamlaka ya ziada.
Washtakiwa katika kesi hiyo, Alphonce Magombola na mama yake mzazi Sophia Mwenda, wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafamilia Beatrice Magombola, binti wa mama huyo.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashitaka katika tukio hilo, Alphonce alimfunga miguu dada yake Beatrice na kumshikilia mikono kisha mama yake, Sophia akamchoma bintiye kwa kisu kwenye titi la kushoto mpaka alipofariki dunia.
Kulingana na ushahidi huo, washtakiwa walitenda kosa hilo kwa kuwa mwanafamilia huyo alitaka kwenda kutoa ushahidi kwenye kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga mwenye mamlaka ya ziada, lakini imerejeshwa Mahakama Kuu.
Mabadiliko hayo yameelezwa mahakamani na mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali, Asiath Mzamiru kesi ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
“Kwa leo tutashindwa kuendelea kwa sababu tunasubiri re-signment (kupangiwa jaji wa kuisikiliza) Mahakama Kuu,” alisema na kuomba kesi iahirishwe ipangwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Ombi hilo halikupingwa na wakili wa washtakiwa, Denis Mniko.
Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo kwa siku 14 akipanga itajwe Desemba 30, 2024.
Washtakiwa walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza Julai 15, 2022 na kusomewa shitaka hilo.
Wanadaiwa kwa pamoja walimuua Beatrice Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi, wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Kesi ilifunguliwa mahakamani hapo kwa hatua za awali ikiwemo kukamilisha upelelezi kwa mujibu wa sheria. Julai 23, 2023 washtakiwa walisomewa maelezo ya mashahidi.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Machi 16, 2020 saa nne asubuhi aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai (sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai -DCI), alipokea taarifa kutoka kwa msiri kuhusu kupotea kwa Beatrice Magombola.
Msiri huyo alidai kumekuwa na taarifa za utata kuhusu kupotea kwake kwani mama mzazi wa Beatrice (mshtakiwa wa pili), anadai amekwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine akiulizwa anadai amekwenda Canada kutibiwa.
Mama huyo hakuweka wazi ugonjwa unaomsumbua Beatrice na taarifa za ugonjwa hazikuwa zikifahamika kwa ndugu wa Beatrice wala baba yake mzazi, isipokuwa kaka yake mkubwa Alphonce (mshtakiwa wa kwanza).
Msiri alieleza Beatrice alikuwa na gari aina ya Vanguard lililokuwa likitumiwa na Alphonce na nyumba yake iliuzwa na Sophia. Ilidaiwa kuna wakati washtakiwa wakihojiwa kuhusu kupotea kwa Beatrice wanakuwa wakali.
Kutokana na taarifa hizo za msiri, Kingai alielekeza kufunguliwa jalada la uchunguzi. Upelelezi ulifanyika na washtakiwa walikamatwa.
Washtakiwa katika maelezo ya onyo wanadaiwa walikiri kumuua Beatrice kwa kumchoma kwa kisu titi la kushoto baada ya Alphonce kumfunga miguu na kumshika mikono, kisha Sophia akamchoma kwa kisu hadi alipofariki dunia.
Baada ya kumuua wanadaiwa waliuzungusha mwili kwa shuka na mkeka na kwenda kuutupa eneo la Zinga, Bagamoyo.
Wanadaiwa kumuua kwa sababu alikuwa anataka kwenda kutoa ushahidi mahakamani Mbeya katika kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa.
Upande wa mashitaka ulieleza unatarajia kuwaita mashahidi 40 akiwemo Kingai na utawasilisha vielelezo 13.
Mahakama ya Kisutu ilihitimisha jukumu lake la kufanya uchunguzi wa awali, hivyo jalada kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji.
Kesi ilirejeshwa Mahakama ya Kisutu isikilizwe ushahidi na Hakimu Kiswaga aliyepewa mamlaka ya ziada, kabla ya kurejeshwa tena Mahakama Kuu.