Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ametoa miezi miwili kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuhakikisha vitambulisho milioni 1.2 ambavyo tayari vimeshatengenezwa vinasambazwa na kuwafikia wananchi.
Waziri Bashungwa amesema hayo leo Desemba 17, 2024 jijini Dar es Salaam katika ziara ya kikazi ya kutembelea na kujionea utendaji wa mamlaka hiyo.
“Ni wajibu wenu (Nida) kuhakikisha kadi hizi mnazifutilia na zinawafikia walengwa ndani ya miezi miwili kuanzia sasa, nitakapo rudi na kuomba taarifa ya kadi hizi zilizozalishwa nataka ziwe zimewafikia walengwa,” amesema Bashungwa
Bashungwa pia ameitaka Nida kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuondokana na tabia ya urasimu, ambapo ameiagiza Menejimenti kuanza kuwachukuliwa hatua baadhi ya watumishi wazembe ambao hawatoi huduma nzuri kwa Watanzania.
Bashungwa amewakumbusha Watanzania kujenga utamaduni wa kujisajili kupata kitambulisho cha Nida mara wanapotimiza miaka 18 na sio kusubiri mpaka kihitajike, ili kuondokana na usumbufu ambao mara nyingi hujitokeza wakati wa usajili wa wanachuo na kipindi cha vijana kujiunga na mafunzo mbalimbali.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uzalishaji wa Vitambulisho Nida, Edson Guyai amesema vitambulisho ambavyo havijawafikia walengwa ni vya wanafunzi na watu waliohama.
Amesema jitihada zinazofanyika ni kukusanya vitambulisho vyote vilivyokaa muda mrefu na kuanza kufuatilia wahusika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuwatumia wananchi ujumbe wa sehemu watakapochukua vitambulisho hivyo.