Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene amezitaka mamlaka za nidhamu kuchukua hatua stahiki na kwa wakati kwa watumishi waliobainika kughushi barua na walioshiriki katika mchakato wa kughushi barua za uhamisho.
Simbachawene ameyasema hayo leo Jumanne Desemba 17, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa idara na vitengo vya utawala rasilimali watu kutoka taasisi na wizara jijini Dodoma.
“Mamlaka za nidhamu zichukue hatua stahiki na kwa wakati kwa watumishi wote waliobainika kuwa na barua za kughushi na walioshiriki katika mchakato wa kughushi barua za uhamisho kwa tarehe zilizobainishwa katika barua za maelekezo,” amesema Simbachawene.
Amesema wamewapa ripoti na wengine wamewaelekeza wachukue hatua stahiki wasisubiri hadi Katibu Mkuu achukue hatua hizo.
Aidha, amewataka wakuu hao kutenda haki kwa wafanyakazi, wakiwasimamia kinidhamu kwa wale wanaozembea kutimiza majukumu yao.
“Katika kizazi hiki cha leo, uwazi wa upashanaji habari uliopo katika dunia na hususan nchi yetu ambayo kila mtu ana intaneti wa kudanganywa hawapo, hivyo twendeni tukafanye kazi tu, tuhudumie wananchi kwani uongouongo hauwezi watu wana majawabu,” amesema.
Aidha, Simbachawene ameonya kuhusu upendeleo wa fursa mbalimbali za kiutumishi na kuwa zipo baadhi ya taasisi watu wanaosafiri ni haohao tu kila wakati.
Amesema moja kati ya maofisa rasilimali watu wanayojifunza ni kurithishana nafasi za kazi, lakini wapo ambao hadi wanastaafu hawajafanya hivyo wanaomba kuongezewa mikataba.
Ameongeza pia kuwa watu wanaofanya uamuzi mbaya ndio wanung’unikaji wakubwa wakistaafu halafu wao ndio wanaomba kuongezewa mkataba.
“Uongezewe mkataba wa nini? Wakati tuna Watanzania milioni 60. Kuna kundi kubwa linafanya ushawishi wa kuongezewa mkataba upi wakati vijana hawana ajira. Tunang’ang’ana na watu wazee kuwaongezea mkataba waje kwenye siasa tukagombee,” amesema.
Naye, Naibu Waziri, Deus Sangu amesema pamoja na kazi inayofanywa na Serikali lakini, bado kumekuwapo na malalamiko kwa baadhi ya watumishi ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanana na mengi ni ya muda mrefu na yapo katika dhamana ya waajiri kisheria, lakini hayashughulikiwi kwa wakati.