Mkataba usitishaji vita Gaza unakaribia – DW – 18.12.2024

Taarifa hizo zimetoka kwa vyanzo hivyo vilivyoarifiwa juu ya mazungumzo yanayoendelea mjini Cairo ambayo ripoti zinasema yanapiga hatua kubwa.

Vyanzo hivyo vilivyonukuliwa na shirika la habari la Reuters vimesema mkataba wa kusitisha vita uko mbioni kupatikana na utafanikisha pia kuachiwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na kundi la Hamas kwa mabadilishano na wafungwa wa Kipalestina wanazuiwa kwenye jela za Israel.

Marekani imeongeza jitihada mnamo siku za karibuni kwa kupigia debe kuharakishwa mkataba wa kusitisha uhasama kabla ya kuondoka madarakani Rais Joe Biden hapo Januari mwakani.

Mkuu wa CIA kuelekea Qatar kusawazisha vipengele vya mkataba vinavyobishaniwa

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Marekani cha Fox News, Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, John Kirby, amesema Washington inaamini kuwa makubaliano yatakapatika hivi karibuni.

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, John Kirby
Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, John Kirby.Picha: Andrew Leyden/ZUMA Press Wire/picture alliance

“Tunaamini – na Waisraeli wamelisema hili – kwamba tumekaribia, na hakuna shaka yoyote kuhusu hilo, tunaamini, lakini vilevile tunakuwa makini na matarajio yetu”, amesema afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani.

“Tumekuwa kwenye nafasi kama hii hapo mwanzo ambapo hatukufanikiwa kuvuka mstari wa mwisho”, ameongeza Kirby akikumbusha matarajio ya miezi iliyopita ya kupatikana makubaliano ya kusitisha vita ambayo hata hivyo yaliambulia patupu.

Hata hivyo vyanzo vinavyofahamu kinachoendelea kwenye mazungumzo ya mji Cairo vimesema mkataba wa kusitisha vita unanukia na utapatikana ndani ya siku chache zijazo.

Duru zinasema Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, William Burns, ambaye anaiwakilisha Washington kwenye mazungumzo hayo ya mjini Cairo, atasafiri kwenda nchini Qatar leo Jumatano kwa mashauriano na waziri mkuu wa nchi hiyo Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani ya kukamilisha vipengele kadhaa vyenye utata kati ya Israel na kundi la Hamas.

Hayo yameripotiwa na Shirika la Habari la Reuters likinukuu duru zinazoaminika. Hata hivyo CIA imekataa kutoka maelezo yoyote juu ya taarifa hizo.

Je, mara hii mkataba wa kusitisha vita utapatikana tofauti na duru zilizotangulia?

Athari za vita kwenye Ukanda wa Gaza
Athari za vita kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Hani Alshaer/Anadolu/picture alliance

Vyanzo viwili vya usalama kutoka Misri vimesema kwamba mashauriano yanaendelea kukamilisha vipengele vichache vinavyoleta ukinzani.

Miongoni mwavyo ni matakwa ya kundi la Hamas ya kupatiwa hakikisho kwamba mkataba wowote wa kusitisha mapigano kwa muda utafuatiwa na makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita kwenye Ukanda wa Gaza.

Maafisa wa Marekani na Israel wameelezea matumaini kwamba majadiliano yanayosimamiwa na Misri na Qatar yanaweza kufanikisha kupatikana makubaliano mwishoni mwa mwezi huu lakini wametahadharisha kwamba mazungumzo hayo pia yanaweza kusambaratika.

Wawakilishi wa Israel walikuwa mjini Doha siku ya Jumatatu, kujaribu kutanzua maeneo yenye mkwamo kati ya nchi hiyo na kundi la Hamas hasa kwenye pendekezo la mkataba lililotolewa na Rais Biden mwezi Mei mwaka huu.

Kumekuwepo na duru kadhaa za mazungumzo tangu mwaka jana ambazo zote zilishindwa hasa baada ya Israel kushikilia msimamo wake wa kutaka kubakia kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza na Hamas wakikataa kuwaachia huru mateka wa Israel hadi vikosi vya Israel viondoke.

 

Related Posts