Dar es Salaam. Baadhi ya makada na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka mikoa mbalimbali, ikiwamo Dar es Salaam wamejipanga leo Desemba 18, 2024 kwenda nyumbani kwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, Mikocheni kumuomba agombee tena nafasi hiyo.
Hadi sasa Mbowe hajaweka wazi kama atawania nafasi hiyo au la.
Mmoja wa waratibu wa mchakato wa kwenda kwa Mbowe aliyeomba jina lake lisitajwe ameieleza Mwananchi Digital kuwa wanajipanga kwenda kuonana na Mbowe nyumbani kwake.
“Tukio la kwanza kwenda nyumbani kwake leo saa tano asubuhi kumuomba agombee uenyekiti wa chama. Kutakuwa pia na viongozi mbalimbali wanaokwenda kumuomba Mbowe agombee tena uenyekiti, akikubali tutakwenda kumchukulia fomu makao makuu.
“Kwa sasa hatujaona mtu mwenye sifa ya kuwa kiongozi zaidi yake. Mbowe atasema atakubali kugombea au la, akikubali ataletewa fomu kwa ajili ya kuijaza,” amesema.
Katika uchaguzi mkuu wa chama hicho wa mwaka 2019 kundi la vijana lilichangisha Sh5.6 milioni na kwenda kumchukulia fomu ya uenyekiti na kumshawishi Mbowe agombee tena nafasi hiyo.
Katika uchaguzi wa Chadema mwakani, tayari pia yapo makundi ambayo yanaendesha michango kwa ajili ya fomu ya Mbowe.
Tayari Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amechukua fomu kugombea nafasi hiyo.
Lissu aliyetangaza nia kuwania uenyekiti wa chama hicho Desemba 12, jijini Dar es Salaam alichukua fomu jana Desemba 17 na anatarajiwa kuirejesha leo.
Alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Mikocheni, Dar es Salaam.
Lissu alifika ofisi za makao makuu ya Chadema saa 6:20 mchana akiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser V8.
Alisema fomu yake imelipiwa Sh1.5 milioni na mwathirika wa tukio la kutekwa, Edgar Mwakabela, maarufu Sativa. Sativa alidaiwa kutekwa Juni 23, 2024 na watu wasiojulikana kisha kuokotwa Juni 27, porini mkoani Katavi akiwa na majeraha kichwani.
Lissu alisema pia baadhi ya wanachama wa Chadema walichanga fedha kwa ajili ya kulipia fomu hiyo.
Akizungumza jana asubuhi katika mahojiano na kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds yaliyofanyika nyumbani kwake Tegeta, Wilaya ya Kinondoni, Lissu alisema hana wasiwasi kupambana na mwenyekiti wake, Mbowe.
“Kitu ambacho wanakiona cha ajabu ni hiki, mara hii makamu mwenyekiti anagombea? Sasa mlitaka achukue nani? Kama siyo makamu mwenyekiti, nani ameandikiwa kuchukua fomu na nani asichukue?
“Kinachoonekana cha ajabu ni hicho tu, kwamba mara hii makamu mwenyekiti wa chama anagombea, lakini mwenyekiti mwenyewe (Mbowe) wala hajasema kama anagombea,” alisema.
Hata hivyo, Lissu alisema hana ugomvi wala vita na Mbowe au viongozi wengine wakuu wa Chadema, ndiyo maana baada ya kutangaza nia ya kuwania uenyekiti, kesho yake waliketi pamoja kwenye kikao cha kamati kuu.
“Ipo wazi tuna tofautiana kimsimamo, kimtazamo wa mambo mengine, lakini kuna mengine mengi tunakubaliana, ndiyo maana tupo chama kimoja,” alisema.