Hesabu za Fadlu kumaliza mwaka kileleni akianza kwa KenGold

BAADA ya wekundu wa Msimbazi, Simba kuwa na siku 18 za uwakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa, hatimaye wanarejea uwanjani katika hekaheka za Ligi Kuu Bara, wakiwa na dhamira ya kurejesha heshima yao na kurudi kileleni.

Leo, Jumatano, wakiwa na morali ya juu, Simba iliyovuna pointi sita katika Kombe la Shirikisho Afrika katika michezo mitatu ya Kundi A, itakutana na KenGold kwenye Uwanja KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam na vijana wa Fadlu Davids watakabiliana na timu inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi.

Awali Simba ambayo kwa sasa ipo nafasi ya tatu, ilikuwa ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 28 lakini kutokana na wapinzani wake ikiwemo Azam kuendelea na ligi wakati wao wakiwa na majukumu ya kitaifa pamoja na watani zao Yanga, walizidiwa kete na Azam FC ambao wapo mbele kwa michezo minne.

Kabla ya mechi ya jana, Jumanne usiku dhidi ya Fountain Gate, Azam ilikuwa ikiongoza ligi kwa pointi 30 sawa na Singida Black Stars.

Hata hivyo, Simba itakuwa na kibarua kizito cha kushinda mechi hii dhidi ya KenGold sambamba na nyingine tatu zinazofuata dhidi ya Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Singida Black Stars ikiwa na lengo la kurejea kwenye usukani wa ligi hiyo.

“Baada ya kumaliza mechi tatu ngumu za kimataifa, sasa nguvu zetu zielekezwe kwenye ligi. Kuna mechi muhimu mbele yetu ndani ya kipindi kifupi, na tunahitaji kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri. Matokeo mazuri kwenye ligi yatakuwa na faida kubwa kwa timu na mashabiki wetu,” alisema Fadlu.

Katika michezo mitatu ijayo ya Ligi Kuu Bara baada ya leo kupambana na Kengold, Simba itakuwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar, Desemba 21, kisha Desemba 24 itarejea nyumbani kukabiliana na Tanzania Prisons huku ikiufunga mwaka kwa kucheza dhidi ya Singida Black Stars ugenini Desemba 28.

Mechi hizi zitakuwa ni mtihani mkubwa kwa Simba, hasa kwa sababu zitakuwa na athari kubwa katika mapambano yao ya ubingwa na inahitaji kushinda ili kuendelea kukalia nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi.

“Tunahitaji kuwa na umoja na dhamira ya kushinda. Mashabiki wetu wanatarajia kuona timu inacheza kwa juhudi kubwa na kupata matokeo bora. Hii ni changamoto kwetu na tunahitaji kujituma ili kuwapa furaha mashabiki wetu. Tunajua kila mchezo ni muhimu na tutapambana hadi mwishoni,” alisisitiza Faldu.

Katika mchezo wa leo dhidi ya KenGold, Fadlu alisema vijana wake wamejiandaa vizuri na mchezo huo licha ya kuwa na wakati mdogo wa maandalizi.

“Tumejivunia wachezaji wetu na kiwango cha uchezaji kilichoonyeshwa katika michezo ya kimataifa, tuna nafasi ya kuimarika zaidi. Ingawa tumekuwa na mechi ngumu na kubwa za kimataifa, hatutaki kuwa na mapumziko kwenye ligi. Tuna dhamira ya kurudi kileleni kwa kushinda kila mechi na mchezo dhidi ya Kengold ni muhimu sana kwetu.”

Katika michezo mitano ya mwisho ya ligi, Simba imeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kushinda, huku wakishinda michezo yote bila kuruhusu nyavu zao kuguswa. Hii ni ishara, safu yao ya ulinzi iko imara, huku wakiwa na uwezo mzuri wa kufunga pamoja na changamoto iliyopo kwa washambuliaji wao wa mwisho.

Katika michezo ya ligi, Simba ilishinda dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), Namungo (3-0), Mashujaa (1-0), KMC (4-0), na Pamba Jiji (1-0). Mabao 10 yaliyofungwa katika michezo hii yanaonyesha jinsi Simba ilivyokuwa katika kiwango bora huku wakifunga kwa wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo.

KenGold, kwa upande mwingine, ina hali ngumu, ikiwa inashika mkia wa msimamo wa ligi na ina pointi sita tu, baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoa sare tatu katika michezo 14 ya ligi. Kengold imekuwa ikifanya vibaya katika ligi, huku wakiruhusu mabao 25 na kushindwa kushinda kwa muda mrefu.

Katika michezo yao mitano ya mwisho, wamepoteza mara tatu dhidi ya Namungo (3-2), Pamba Jiji (1-0) na Tanzania Prisons (1-0) , wakitoa sare mbili tu dhidi ya Dodoma Jiji (2-2) na Coastal Union (1-1). Kwa hivyo, ni wazi Simba ni miongoni mwa timu ambazo Kengold itakuwa na wakati mgumu.

Hata hivyo, Kocha wa KenGold, Omary Kapilima ameonyesha atapambana kwa kila hali akisema: “Ligi Kuu ni changamoto kubwa, lakini hatutakubali kupigwa ovyo. Tunaenda kwa imani, licha ya changamoto zetu. Simba ni timu bora, lakini sisi tutapambana kwa nguvu zetu zote,” alisema Kapilima.

Moja ya silaha kubwa ya KenGold ni mchezaji wao Ibrahim Joshua, ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwa timu hiyo, akifunga mabao manne msimu huu. Joshua, ambaye ana uzoefu wa kucheza soka la kulipwa Kenya, ni mmoja wa wachezaji wanaoweza kuleta changamoto kwa Simba kwa kutumia uzoefu wake.

Simba, inajivunia kiwango cha Kibu, ambaye ameonyesha ufanisi mkubwa katika michuano ya kimataifa, akifunga mabao mawili katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya CS Sfaxien. Kwa upande mwingine Simba inaye Charles Jean Ahoua, ambaye ana mabao matano na asisti nne kwenye ligi nyota hao wanatarajiwa kuonyesha umahiri wao katika mchezo huu.

Related Posts