Mwenyekiti mpya CUF kujulikana leo

Dar es Salaam. Jawabu kuhusu kuendelea au kukoma kwa uongozi wa Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi ya uenyekiti wa CUF Taifa, linatarajiwa kupatikana leo, baada ya matokeo ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Katika uchaguzi huo unaohusisha kuwapata viongozi wa chama hicho kwa ngazi za kitaifa, Profesa Lipumba anachuana na makada wengine wanane waliopitishwa kuwania nafasi hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa CUF bara, Maftah Nachuma ni miongoni mwa makada wanaogombea nafasi hiyo.

Sambamba naye, wamo Ali Hamisi, Athumani Kanali, Juma Nkumbi, Nkunyuntila Chiwale, Wilfred Rwakatare (Mbunge mstaafu wa Bukoba Mjini) na Chifu Yemba (aliyewahi kuwania urais kwa tiketi ya ADC 2020).

Kiu waliyonayo wengi ni kujua iwapo Profesa Lipumba atafanikiwa kutetea nafasi yake aliyohudumu kwa miaka 25 tangu 1999 au ndiyo utakuwa mwisho wa enzi ya uenyekiti wake.

Hali ya ukumbini kabla ya uchaguzi

Mkutano huo wa uchaguzi, umetanguliwa na mkutano mkuu wa kawaida wa chama hicho, uliohusisha hotuba za viongozi mbalimbali wa kitaifa.

Mkutano huo mkuu, ulihudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kikiwemo CCM, Chadema na ACT Wazalendo.

ACT Wazalendo iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu huku Chadema ikiwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Benson Kigaila

Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid ndiye aliyeiwakilisha CCM katika mkutano huo, ambao pia unahusisha kufanyika kwa uchaguzi wa nafasi za kitaifa.

Lakini, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ndiye aliyekuwepo kwa niaba ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Saa 5:32, Kamati ya Uchaguzi iliitwa mbele kuanza utekelezaji wa majukumu ya kuratibu uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo iliyoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF, Mashaka Ngole alianza kwa utambulisho wake binafsi na wajumbe wake wanne.

Amri ya watu wote kutoka ndani ya ukumbi ili kupisha uhakiki wa wajumbe halali wa kuingia ukumbini lilifuata.

Tukio hilo, lilifuatiwa na kuchaguliwa kwa mwenyekiti wa muda atakayeongoza shughuli zote hadi pale atakapopatikana Mwenyekiti wa taifa baada ya matokeo.

Kama ilivyo katika chaguzi mbalimbali, wapiga debe kinyemela hawakukosekana, walishuhudiwa wakizunguka huku na kule kuwaombea kura wagombea wanaowavutia.

Kitakachokushangaza, hadi maofisa itifaki wa chama hicho, walikuwa sehemu ya kampeni za chinichini za wagombea, wengi wakishawishi Profesa Lipumba achaguliwe tena.

Hadi saa 6:19 uhakiki na kuwaingiza ndani ya ukumbi wajumbe halali wa mkutano huo kwa ajili ya kumpata mwenyekiti wa muda, haukuwa umekamilika.

Kwa mujibu wa chama hicho, chaguzi za viongozi wote zitafanyika leo na mkutano wa kesho utahusisha hotuba za viongozi pekee.

Related Posts