Wiki iliyopita nilizungumzia namna Katiba ya Zanzibar inavyouvunja muungano kwa kuiita Zanzibar ni nchi, na jinsi Katiba ya Zanzibar ilivyopoka mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT).
Leo tutaangalia namna Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilivyopoka mamlaka ya Bunge la JMT kwa kutunga sheria za muungano na jinsi Mahakama Kuu ya Zanzibar ilivyopoka mamlaka ya Mahakama Rufaa ya JMT ambayo ndiyo mahakama ya mwisho ndani ya Jamhuri.
Kabla sijakwenda kwenye mada ya leo, naomba kuwapa mrejesho wa yatokanayo na mada ya wiki iliyopita, huu ni mchango wa msomaji wa gazeti la Mwananchi, aliyejitambulisha kwa jina la Kapteni Ibrahim Bendera, hapa ninamnukuu:
“Habari za leo. Nimeiona makala yako kwenye Mwananchi la leo, nadhani nikupe mawazo yangu: Kwanza, duniani kuna aina tatu kuu za muungano ambazo ni total union (muungano kamili) federation (shirikisho) na confederation (shirikisho).
Pili, aina ya muungano wa Tanzania ni mseto wa total union (Tanganyika); na federation (Zanzibar). Kwa hiyo kwa Tanzania Bara Serikali ni moja, kwa Zanzibar serikali ni mbili.
Zanzibar ni nchi yenye Katiba ya 1984 (kama inayorekebishwa) na inatambuliwa kwenye aya ya 102(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ukisoma aya ya kwanza ya Katiba ya JMT, inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano”, ya Kiingereza inasema: Tanzania is one State and is a sovereign United Republic.
Hili neno ‘sovereign’ (dola huru) halipo kwenye Katiba ya Kiswahili.
Makubaliano ya Muungano yanafanana na makubaliano ya Muungano wa Scotland na England kuanzisha Great Britain. Scotland wana Bunge lao; Bunge la England limekuwa Bunge la Great Britain.”. Mwisho wa kunukuu.
Namshukuru sana msomaji wetu, Kapteni Bendera, maoni yake ni msaada mkubwa kwangu na wasomaji wangu, kwa sababu, kiukweli, elimu inayotolewa kuhusu huu muungano wetu adhimu na adimu ni finyu sana, hivyo elimu hii imenifungua macho zaidi kuendelea kuelimisha kuhusu muungano.
Sasa turudi kwenye Katiba ya Zanzibar na Katiba ya JMT. Katiba ya Zanzibar haikuishia hapo, katika Ibara ya 2A inatamka kwamba “kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.”
Masharti haya ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 2(2) ambayo inatamka: “Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge: Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo.”
Ibara hiyo inapoka madaraka ya Rais wa JMT, kupoka madaraka ya Rais ni kosa la uhaini.
Ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar, inatamka kwamba: “Hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika. Ibara hii inaeleza zaidi, pale sheria ndogo inapoundwa kwa mujibu wa uwezo uliowekwa chini ya kijifungu cha 132(1) na (2) itatumika tu pale itakapotimiza shuruti zote zilizowekwa kwa matumizi ya sheria mama kama ilivyoainishwa katika kifungu hiki.
Masharti haya ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 64 ambayo inatamka kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano ndilo lenye mamlaka ya kutunga sheria kwa mambo ya Muungano (Bara na Zanzibar) na yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara.
Ibara hiyo imepoka madaraka ya Bunge la JMT ya kutunga sheria za mambo ya muungano na kulifanya Baraza la Wawakilishi kuwa ndilo lenye mamlaka ya juu kuhusu muungano.
Katika Ibara ya 24(3) ya Katiba ya Zanzibar: “Rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu (Zanzibar) katika shauri lililofunguliwa dhidi ya masharti ya sura hii ya Katiba yatasikilizwa na Mahakama Kuu (Zanzibar) mbele ya majaji watatu, na uamuzi wao utakuwa ni wa mwisho na hautakatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.”
Ibara hii ni kinyume cha Ibara ya 117(1) na (4) ambayo inatamka kwamba Mahakama ya Rufani ndiyo yenye Mamlaka ya juu ya kutoa haki nchini na uamuzi wake ni wa mwisho, hivyo Mahakama Kuu ya Zanzibar, kupoka mamlaka ya Mahakama ya Rufani ya JMT na Jaji Mkuu wa Zanzibar kuwa ndiye mkubwa kuliko Jaji Mkuu wa Tanzania.
Ukiondoa uwepo wa nchi, Katiba ndio nyaraka muhimu kuliko nyingine yoyote, haiwezekani, Katiba ya JMT isiitambue Katiba ya Zanzibar, huu ukiwa ni mwaka wa 14. Miongoni mwa haki muhimu za Zanzibar, ni haki ya Katiba yake kutambuliwa na Katiba ya JMT. Hali hii lazima irekebishwe.