Jinsi wananchi wanavyobadili desturi matumizi ya mikoko-2

Mikoani. Ilizoeleka kwa muda mrefu kuwa jamii za pwani hutegemea miti ya mikoko kwa ajili ya ujenzi, kutengeneza majahazi na mitumbwi, kuni, mbao za kutengenezea samani na matumizi mengineyo.

Hata hivyo, kwa sasa matumizi ya mikoko yamedhibitiwa, hivyo wananchi wanalazimika kubadilisha mazoea ya matumizi ya mikoko kutokana na uharibifu wa miti hiyo.

“Hapo awali mikoko ilikuwa inakatwa kwa ajili ya ujenzi na matumizi mengine, tukaona tuweke mikakati,” anaeleza Mdachi Bwatumu kutoka Kijiji cha Mwaboza, wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga.

Anasema umasikini wa kipato ulikuwa pia sababu ya uharibifu wa misitu na ndipo walipopatiwa njia mbadala na Shirika la Mwambao Coastal Conservation Network na sasa wameanza kubadilisha tabia.

“Mwambao walipokuja mwaka 2022 walituwezesha kwa mafunzo na vifaa tukaanza kupanda mikoko, tunashukuru kwa elimu tuliyoipata na sasa tunaanza kuona mafanikio.

“Tunaona sasa hivi miche ya mikoko imekuwa mingi na tunapanda na kuziba yale maeneo yaliyokatwa,” anasema.

Sofia Tapo wa kikundi hicho anasema tangu vikundi vimeanzishwa wamepata manufaa, ikiwa pamoja na mitaji ya biashara zzao.

“Tunashukuru pia kwa kupatika fedha za Mfuko wa Utunzaji wa rasilimali za bahari, Sh2.1 milioni kwa kila kikundi. Kwa hiyo tunakopeshana ili kukidhi maisha yetu.

“Baada ya kupata elimu hii, kwa vijiji ambavyo hawana miche, wanakuja kununua na sisi tunapata kipato. Motisha yangu ni kuona tu mazingira yanaboreshwa, kwa sababu tunajua kuna athari kubwa zimewakumba watu wengine.”

Mbali na kuwapa mafunzo, shirika hilo linatoa mitaji ya kibiashara kwa wanavikundi ili kufanya ujasiriamali wakati wakitunza mazingira.

Akieleza uratibu wa shirika hilo, mratibu wa shirika hilo wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga, Fakhi Sheha anasema awali mwaka 2017 walianza kupambana na uvuvi haramu wa kutumia baruti na sasa wamejikita kwenye utunzaji wa mikoko.

Kwa upande wa mikoko anasema waliangalia athari wanazopata wananchi kwa kukatwa mikoko.

“Kwa hapa Mkinga tulianza na kijiji cha Dumbani, lakini tumeendelea na kijiji cha Nyasini na Moa, Mwaboza, Zingibari, Boma Sukutumi na Boma Kichakamimba. Kwa hiyo tukaanza kuwahamasisha wananchi kuhifadhi mikoko,” anasema.

Anasema kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wameunda kamati za mazingira na vikundi vya mazingira.

“Tumechukua baadhi ya wanavijiji kupitia vikundi vyao tumewapeleka Mombasa kupata mafunzo ya kutunza na kurejesha mikoko, kuandaa vitalu, aina za mikoko kwa sababu huwezi kufanya kitu bila kujua asili yake.

“Baada ya vijana wale kujifunza wamerudi kwenye maeneo yao na wameanza kuotesha mikoko kwenye vitalu wakiangalia sehemu zilizoathirika na wanarejeshea,” anasema.

Hata hivyo, anasema kulikuwa na changamoto wakati wa kupanda, kwani baadhi ya miche ilikuwa inakufa, hivyo ikabidi watafute wataalamu wa kuangalia na kuwashauri aina ya mbegu na maeneo mahususi ya kupanda.

“Kwa sasa wameotesha miche kwenye vitalu ambavyo licha ya kurejesha tu, pia wanauza kwa mashirika mengine, kwa mfano hapa Mwaboza wameshauza mara tatu.

“Kuna mashirika yanakuja yanainunua miche kwa lengo la kurejeshea, halafu wakishaichukua wanakwenda kupanda kwenye maeneo hayo hayo ya vikundi, kwa hiyo ni faida mara mbili kwa sababu nguvukazi imetoka kijijini na mikoko inarudi pale pale kijijini,” anasema.

Ili kuwapa motisha, anasema wameanzishia mfuko wa kutunza mazingira ambao vikundi hupewa Sh2.1 milioni kwa kila kikundi ambazo wanakopeshana bila riba kwa ajili ya kazi zao za kutunza mazingira.

Wanavijiji wataka elimu zaidi

Wakizungumza kwa nyakati tiofauti, baadhi ya wanavijiji wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi wamesema pamoja na kuanzisha vikundi bado wanahitaji elimu ya utunzaji mazingira ya bahari.

Mwanakikundi wa Somanga Majongoo, Salome Chacha anasema kikundi chao kilisajiliwa Septemba 2023, wakijishughulisha na ufugaji wa majongoo kuchakata samaki, kilimo cha mwani na upandaji wa mikoko.

“Kikubwa tunahitaji elimu, kwa sababu hata huku kupanda mikoko, siyo kwamba tunajua aina za miti na mahali inapotakiwa kupandwa. Pia tunahitaji vifaa kama mabuti kwa ajili ya kukanyaga kwenye matope yale, maana watu wengi wanakuja miguu peku. Mpaka sasa tumepanda miche 500. Tunashukuru miti yote hii inaendelea vizuri,” anasema.

Katibu wa kikundi cha Marendego Mazingira Group, Maulid Ally Mtomboni, anasema licha kikundi chao kupata miche 9,500 ya mikoko, bado wanahitaji elimu zaidi na uwezeshaji wa fedha ili kuendeleza mradi.

“Kama taasisi tunakosa elimu ya jinsi ya kupanda mikoko. Tumeanza kupanda mikoko tangu Mei, lakini tunapata changamoto ya baadhi ya mikoko kukauka, kwa hiyo tunahitaji elimu ya kutuwezesha kujua aina gani ya mikoko ipandwe wapi.

“Tumeshapanda mikoko 9,500,500 aina ya michu, 4,000 ni mkandaa na mikanga ni 5,000, hivyo tunaomba kujengewa uwezo na kupata miradi kama kutuwezesha kufuga nyuki ili tupate kipato,” anasema.

Katika kuwawezesha wanavijiji kulinda miti ya mikoko, hivi karibuni Shirika la Kuhifadhi Mazingira la Kimataifa (WWF) lilitoa Sh106.7 milioni kwa baadhi ya wananchi katika mikoa ya Pwani na Lindi kwa lengo la kuwawezesha kufanya ujasiriamali na kuhifadhi misitu ya mikoko.

Fedha zilitolewa Novemba 4, 2024 kwa vikundi 10 kwa ajili ya kutunza mazingira ya bahari kutoka wilaya za Kibiti na Mafia, Mkoa wa Pwani na Kilwa mkoani Lindi.

Mkuu wa Programu ya Mambo ya Bahari (Marine) kutoka WWF, Dk Modesta Medard anasema fedha hizo zimewekwa moja kwa moja kwenye akaunti za vikundi.

“Hivi vikundi vinajikita katika kutunza mazingira kwenye vijiji vyao, ikiwa pamoja na ufugaji wa nyuki, usimamizi wa rasilimali za vuvuvi, pia kuna Vicoba.

“Katika fedha hizo, Wilaya ya Kibiti ina vikundi viwili vinavyopata Sh21 milioni, Kilwa inapata Sh43.7 milioni, Mafia Sh42 milioni, jumla inakuwa Sh106.7 milioni,” anasema.

Kwa upande wa Bagamoyo, Mhifadhi Misitu Mwandamizi wa TFS, Ally Chaligha anasema wanapambana kulinda msitu wa mikoko.

“Katika Wilaya ya Bagamoyo tuna msitu wa mikoko wenye ukubwa wa hekta 5,636 na una urefu wa kilomita 100 kuanzia Mapinga Mto Mpigi hadi Saadani.

“Changamoto ni watu kuingia na kukata miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali na tunatoa elimu kwa wananchi wanaopakana na msitu huu. Tumekuwa tukipanda miti kwa kushirikiana na ofisi za Serikali za Mitaa, Mkurugenzi na mashirika binafsi,” anasema.

Katika kushirikisha wananchi, anasema wameunda vikundi kupitia kamati za maliasili za vijiji kwa Kata za Kisutu na Mapinga.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts