Dar es Salaam. Mwili wa John Tendwa, aliyewahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini utazikwa Desemba 20, 2024 katika makaburi ya Kondo, Tegeta jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, William Tendwa maombolezo yanaendelea nyumbani kwao Kibamba Hospitali.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 18, William amesema mwili wa baba yake utaagwa kitaifa kesho Desemba 19, katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kisha utapelekwa nyumbani kwake.
Tendwa alifariki dunia jana Desemba 17, 2024 saa nane usiku akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Wakimzungumzia Tendwa, baadhi ya wanasiasa wamesema alitenda kazi kwa uwazi. Alihudumu kama msajili wa vyama vya siasa kati ya mwaka 2001 hadi 2013.
Wawakilishi wa vyama vya siasa waliomzungumzia Tendwa ni kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) ACT Wazalendo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita amesema, Tendwa alikuwa tayari kukaa meza moja na vyama vya siasa kunapokuwa na mgogoro.
“Enzi zake hakukuwa na mfululizo wa barua za vyama kufutwa, nakumbuka wakati tupo CUF tuliwahi kumfungia ndani ya ofisi tulipokuwa na mijadala mikubwa na ofisi yake, alikuwa tayari tuzungumze naye na kujenga uelekeo,” amesema.
Amesema vyama vya siasa enzi ya utawala wake vilikuwa huru kupigania mabadiliko bila kupata tishio lolote la kuhojiwa na ofisi ya msajili.
Mchinjita amesema wakati wa utawala wa Tendwa ndani ya ofisi ya msajili, sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2009 na Sheria ya matumizi ya fedha ya 2010 zilipitishwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila amesema Tendwa alikuwa mkweli.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud amesema Tendwa alimfahamu mwaka 1970 wakiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akijipambanua kuwa kama mtu mkarimu.
“Alipokuwa msajili ndipo siasa zilipamba moto baina ya CCM na CUF upande wa Zanzibar, hata kukiwa na mgogoro alikuwa akitenda kama hakuna mgogoro kwa nafasi yake alitenda haki na hakuacha makovu,” amesema.
Kada wa CCM, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Mabodi amesema Tendwa alikuwa na msimamo na mzalendo.
“Hakubagua vyama, alikuwa na msimamo hata mbele ya Rais, alipomaliza muda wake tulikuwa tunamuendea alikuwa anatoa ushauri,” amesema.
Dk Mabodi amesema Tendwa wakati wake ndiko kulianzishwa muungano wa vyama vya upinzani, visivyo na wabunge bungeni na vilivyo na wabunge.
Mbali na hayo amesema wakati wa utendaji wake alisimama katikati ya vyama vya siasa na alikuwa na maono kwenye utawala wake.
Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amesema Tendwa alipenda uwazi na alitenda haki kwa vyama vya siasa.