Shinyanga. Mkazi wa Kata ya Mwendakulima, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Happyness Khalfan (30), anadaiwa kukatwa mkono wa kushoto na mume wake, Charles Peter, baada ya kuchelewa kurudi nyumbani.
Akisimulia tukio hilo, Happyness anasema lilitokea Jumapili Desemba 15, 2024 na sababu ya kujeruhiwa ni baada ya kumuomba mumewe ampeleke hospitali kwa kuwa alikuwa anaumwa.
Hata hivyo, amedai kuwa mumewe alikataa kumpeleka hospitali, badala yake alimwambia angempeleka kwa mganga wa kienyeji Jumanne (Desemba 17, 2024).
“Nikaona nazidi kuumwa nikaamua kutoka kwenda kutafuta matibabu, lakini sikumwambia na nikachelewa kurudi nyumbani. Niliporudi akawa amekasirika akachukua panga kisha akanikata mkono wa kushoto. Hakutaka twende hospitali, alisisitiza twende kwa mganga,” amedai Happyness na kuongeza:
“Baada ya maumivu kuongezeka nikawa napiga kelele majirani wakasikia wakaja wakanichukua wakanipeleka kituo cha afya.”
Akizungumza na Mwananchi Dijital leo, mmoja wa majirani zake Sarah Paulo amesema alisikia sauti ya jirani yake huyo akilia kutokana na maumivu aliyoyapata.
“Nilipoenda nyumbani kwake nilikuta amejeruhiwa vibaya na mkono wake ukivuja damu nyingi. Tukaitana majirani tukatoa taarifa kwa mtendaji wa kata halafu tukampeleka hospitalini. Lakini mumewe alitoroka hatukumuona tena na mpaka sasa hajapatikana anatafutwa na polisi,” amedai Paulo.
Mtendaji wa Kata ya Mwendakulima, Vicent Ndesekio amelaani vikali tukio hilo huku akiisihi jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, bali ifuate utaratibu wa kusuluhisha migogoro ya kifamilia kwa njia halali.
“Natoa wito kwa watu kuacha kujichukulia sheria mkononi. Migogoro inapotokea ni muhimu kufuata taratibu zilizopo ili kuepusha vitendo vya kikatili kama hiki,” amesema Ndesekio.
Naye Ofisa Kliniki Mwandamizi wa Kituo cha Afya cha Mwendakulima, Leonard Mabula amethibitisha kumpokea Happyness akiwa amejeruhiwa vibaya.
“Mgonjwa Happyness Khalfan tumempokea akiwa na jeraha kubwa mkononi lililosababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali na alikuwa akivuja damu nyingi. Hali yake kwa sasa inaendelea vizuri kiasi lakini kama hali ikibadilika itabidi tumuhamishie Hospitali ya Manispaa ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu zaidi,” amesema Mabula.
Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ambaye amesema uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo na mtuhumiwa bado hajakamatwa.
“Chanzo cha tukio bado kinachunguzwa, ingawa mlalamikaji amesema kilitokana na kuchelewa kurudi nyumbani. Mtuhumiwa ambaye alitoroka baada ya tukio tunaendelea kutafuta,” amesema Kamanda Magomi.