Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ameahidi kushughulikia changamoto za vyombo vya habari na waandishi wa habari, ikiwamo Sera ya Habari na Utangazaji inayotaka mwekezaji wa nje ya nchi kumiliki asilimia 49 na mzawa asilimia 51.
Changamoto nyingine ni kuyumba kwa uchumi wa vyombo vya habari, waandishi wa habari kukosa mikataba ya ajira, mafao ya uzeeni na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano kulikosababisha hadhira kupungua kwenye vyombo vya habari vya asili.
Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Desemba 18 alipokuwa akizungumza na wadau wa habari jijini Dar es Salaam, akisema Rais Samia Suluhu Hassan alipomteua alimwagiza kushughulikia kero hizo.
Amesema vyombo vya habari vimeathiriwa kiuchumi ikiwemo kupungua kwa mapato kutoka kwenye matangazo na gharama kubwa za uendeshaji.
“Sera yetu ya Habari ya mwaka 2003 katika kifungu cha 3(2) inaelekeza kuwa wawekezaji katika sekta ya habari kutoka nje ya Tanzania wanapaswa wawe na ukomo wa asilimia 49, huku ikitoa nafasi kwa wawekezaji wa ndani kuwa na asilimia 51.
“Serikali inatambua changamoto hizi na tutaendelea kutafuta njia za kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa huduma kwa ufanisi,” amesema.
Amesema kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kumesanbabisha kuongezeka kwa ushindani wa hadhira kati ya vyombo vya habari vya asili na mitandao.
“Hii imetokana na kutokana tabia ya hadhira kupungua kutoka kwenye radio, televisheni na magazeti na kutumia zaidi mitandao ya kijamii kwa sababu ya kuuharaka wa kupata habari,” amesema.
Amesema pia akili mnemba imeongeza mabadiliko hayo.
Ametoa wito kwa vyombo vya habari kubadili mtazamo ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia ili yawe na mafanikio.
Kuhusu uchumi wa waandishi wa habari, amekubaliana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi waandishi wa habari (Jowuta), Suleiman Msuya kuwa waandishi wengi hawana mikataba ya ajira, jambo linalowafanya wakose uhakika katika kazi wanazofanya.
Kuhusu hilo: “Nyingine ni kukosekana kwa bima za afya na mafao ya uzeeni. Waajiri tutafute ubunifu, tukae na NSSF (Shirika la Hifadhi za Jamii), tuangalie waandishi wa habari wenye mikataba na wasio na mikataba ili kuangalia wazee hawa wawe na heshima,” amesema.
Amesema hata Rais Samia Suluhu Hassan anatambua kuwepo kwa changamoto hizo na ndio maana alipomteua alimtaka azishughulikie.
“Desemba 10 wakati Rais ananiapisha kule Tunguu Zanzibar alinielekeza kushughulikia changamoto za waandishi wa habari,” amesema.
Kuhusu kamati iliyoundwa kuangalia uchumi wa vyombo vya habari, amesema ripoti yake inafanyiowa kazi.
Akieleza mafanikio katika sekta hiyo, Profesa Kabudi amesema ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229, akisema Serikali ilikutana na wadau na kufanya marekebisho ikiwemo kuwaondolea wamiliki wa mitambo ya uchapishaji katika masuala ya kashfa na uchochezi kwa kuwa hawana uwezo wa kuingilia maudhui.
Ametaja pia hatua ya kuwaongezea uhuru wanahabari kutokuwa na hofu za kijinai kwa makosa ya kashfa.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna mapendekezo 12 waliyopeleka ya kuboresha Sheria ya Huduma za Habari hayakufanyiwa kazi.
“Mwaka jana maboresho 21 tuliyoyaomba, tisa yalikubalika yakapitishwa na Bunge lakini 12 yalitolewa maelezo kwamba yaende kwenye Sera ya Habari ya 2003, kwa hiyo tunaamini chini ya uongozi huu mpya mapitio hayo yataharakishwa,” amesema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ameitaka Serikali kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari kwa kuwa bado kuna marekebisho hayajakamilishwa.
“Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo kupitia kifungu cha 9 na 10, bado anayo mamlaka ya kuitisha au kufungia chombo cha habari bila kupitia taasisi zilizoanzishwa za kitaaluma. Hii bado inatutoa doa, huu woga unatoka wapi?” amehoji.