Mbowe ataka saa 48 kuamua hatima yake Chadema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewaomba viongozi, wanachama na makada waliofika nyumbani kwake kuwa wampe saa 48 za kutafakari ombi lao la kumtaka kuwania nafasi hiyo.

Pia, amewaeleza kuwa hataingia kwenye vita itakayokibomoa chama hicho bali ataingia kwenye vita itakayokijenga.

Mbowe ameyasema hayo leo Jumatano, Desemba 18, 2024 wakati akizungumza na wanachama hao nyumbani kwake, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

“Nimesikia ombi lenu, nawaomba mnipe saa 48 za kutafakari kisha nitazungumza na wahariri wa vyombo vya habari Jumamosi (Desemba 21, 2024) hapahapa nyumbani kutoa msimamo wangu.

“Ninachowaahidi kuwa sitaingia kwenye vita itakayokipasua chama, nitaingia kwenye vita itakayokijenga chama chetu. Kuanzia sasa hadi Jumamosi nitakuwa nafuatilia kwa karibu mambo yanavyokwenda, nikiona chama kinakwenda shimoni, Kamanda nitaingia mzigoni,” amesema Mbowe.

Mbowe amejitenga na mpango wa baadhi ya wanachama wa chama hicho waliokusanyika nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam wakimtaka achukue fomu ya kugombea tena nafasi hiyo.

Hata hivyo, amesema asingeweza kuwakatalia ombi lao na kudokeza kuwa moja ya masharti waliyompa ni kutokutoka ndani kuwasubiri.

“Viongozi wenzangu, kuja kwenu kwangu kwa wingi huu kwa gharama zenu, mwingine anaweza kufikiria ni mpango wa Mbowe. Siyo mpango wa Mbowe, na nimekuwa napata si tu mialiko, nimekuwa napata rai mbalimbali, matamko na nafuatilia sana vyombo vya habari, naona ninavyonyukwa huko, unavumilia lakini huweki kinyongo. Nimekuwa vilevile na wakati mgumu na familia yangu mwenyewe, wananiambia, baba inatosha toka achana na siasa…,” amesema Mbowe.

Related Posts