Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa amemuelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura kufanyia kazi mambo matatu kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Mambo hayo yanahusu usalama barabarani, uhujumu wa miundombinu na ulinzi na usalama wa raia.
Ametoa maelekezo hayo leo Desemba 18, 2024 katika hotuba kupitia vyombo vya habari kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Ameelekeza kuimarishwa ulinzi kwenye nyumba za ibada, kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani na kuimarisha doria kwenye njia kuu usiku na mchana, kwa mujibu wa sheria, bila kumwonea au kumpendelea mtu yeyote.
“Kila mmoja wetu akifuata sheria za usalama barabarani na kufanya matumizi sahihi ya barabara, tutasherehekea sikukuu hizi kwa usalama, amani na utulivu kwa kuwa safari bila ajali inawezekana,” amesema.
Amesema taarifa za ajali mbalimbali zimeonyesha dosari kwa baadhi ya vizuizi na vituo vya ukaguzi barabarani, kutozingatia matumizi sahihi ya barabara, hivyo kusababisha ajali.
“Jeshi la Polisi lishirikiane na Tanroads na Tarura, likague maeneo yote nchini yenye vizuizi au vituo vya ukaguzi kuangalia kama vimewekwa kwa kuzingatia sheria na tahadhari ya usalama kwa watumiaji wengine wa barabara,” amesema.
Ameagiza pale itakapokutwa vizuizi au vituo vya ukaguzi vimewekwa bila kuzingatia taaluma na uzingatiaji usalama wa watumiaji wengine wa barabara, wakutane na taasisi au mamlaka husika ili kuviondoa katika maeneo hatarishi na kwa pamoja kukubaliana maeneo sahihi ya kuweka vituo hivyo.
Mbali na hayo, amezungumzia matukio ya uhalifu yanayohusisha uhujumu wa miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), reli ya kisasa (SGR) na miundombinu ya barabara (zikiwemo alama na taa za barabarani).
Amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote yule atakayebainika kuhusika na uhujumu wa miundombinu.
“Serikali imewekeza kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya kujenga na kuendeleza miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi. Nampongeza IGP Camillus Wambura na Jeshi la Polisi kwa ujumla, kwa kuanzisha operesheni maalumu ili kupambana kwa weledi na wezi na wahujumu wa miundombinu ya Tanesco, SGR, barabara na miundombinu kwa ujumla,” amesema.
Ameagiza operesheni hiyo isiwe tu kwa mikoa michache, bali iwe endelevu na kwa mikoa yote nchini.
“Watuhumiwa wanaokamatwa, Jeshi la Polisi lihakikishe upelelezi unakamilika mapema na wahusika wanafikishwa katika vyombo vya sheria iweze kuchukua mkondo wake,” ameagiza.
Mbali na hayo, ameagiza Jeshi la Polisi kuwa mstari wa mbele kupinga na kupambana na vitendo vya rushwa kwa vitendo.
“Wale wachache ambao si waaminifu, nawaahidi wananchi kwamba hatua kali zitaendelea kuchukuliwa, kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Amesema imekuwa ni utamaduni na desturi ndani ya nchi, kusafiri katika kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, kwa lengo la kuwatembelea na kuwasalimia ndugu na marafiki, vyombo mbalimbali vya usafiri, vikitumika yakiwemo magari binafsi, ya abiria na ya mizigo.
“Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wasafiri na wasafirishaji, kuzingatia na kuheshimu sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazoepukika, ambazo mara nyingi zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na hata kusababisha ulemavu kwa ndugu na wananchi wenzetu,” amesema.
Amesema yapo matukio ya ajali yanayotokana na uzembe wa madereva au wamiliki wa magari kutofanyia matengenezo ya mara kwa mara vyombo hivyo vya usafiri.
Ametoa mfano wa ajali ya Desemba 3, 2024 katika eneo la Kihanga, wilayani Karagwe mkoani Kagera, watu saba walifariki dunia papo hapo na majeruhi tisa.
Nyingine amesema ni iliyotokea usiku wa kuamkia leo Desemba 18, 2024 eneo la Mikese, Mkoa wa Morogoro, ambayo watu 15 wamepoteza maisha na wengine saba kujeruhiwa.
“Natoa wito kwa wasafirishaji na watumiaji wote wa vyombo vya moto, kufanya ukaguzi na matengenezo ya vyombo vya moto kila inapopaswa,” ameagiza.
Bashungwa amewaonya wenye tabia ya kuendesha vyombo vya moto ilimradi tu chombo kinawaka na kutembea, kwenda mwendokasi na kupuuza speed limit, wanaojaza abiria kupita kiasi, wanaokunywa pombe na kuendesha vyombo vya moto na tabia nyingine za aina hiyo zinazokiuka sheria za usalama barabarani akiwataka kuziacha kwani zinahatarisha maisha ya Watanzania.
“Ole wake atakayebainika kusababisha ajali za kizembe, Serikali haiko tayari kuona maisha ya Watanzania yanawekwa rehani, kwa uzembe wa watu wachache.
“Hatuko tayari kuacha tabia za kizembe ziendelee kupoteza maisha ya watu na wengine kupata ulemavu, huku sheria za kudhibiti uzembe zikiwa zipo. Tutachukua hatua kali kwa madereva na wasafarishaji wazembe,” amesema.
Amewaomba wasafiri kutoa ushirikiano na kuunga mkono jitihada hizo ili kuwa salama wanapokuwa barabarani.
“Nitoe tahadhari kwa familia zinazotumia magari yao binafsi kufanya matengenezo ya magari kabla ya safari na kuacha utamaduni wa kuchukua mtu yeyote ambaye hana taaluma ya udereva wala leseni na hajapitia mafunzo ya kuendesha magari kwa kukwepa gharama. Kila familia ichukue tahadhari, hususani tunapoelekea mwisho wa mwaka,” amesema.
Akizungumzia ulinzi wa watoto wakati wa sikukuu amesema upo utamaduni wa wazazi kuwaacha waende sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea, ikiwemo maeneo ya ufukweni au kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo ya watoto, huku wakiwa peke yao.
“Niwaombe wazazi kuwalinda watoto na kutoruhusu kwenda kutembea siku za sikukuu wakiwa peke yao. Tumeshuhudia madhara mengi yakiwapata watoto hususani siku za sikukuu wanapokuwa peke yao,” amesema.
Akizungumzia mvua zinazoendelea katika baadhi ya maeneo nchini, amesema pamoja neema ikiwemo ustawi wa kilimo na mazingira, mvua kupita kiasi husababisha kukatika kwa mawasilianao ya barabara na
maeneo mengine kujaa maji.
“Naomba kutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kubwa katika maeneo yenye mikondo ya maji inayokatiza barabarani. Wazazi na walezi wenzangu tusiache watoto wetu kuvuka pekee yao kwenye maeneo hatarishi ya maji au kuogelea kwenye madimbwi yanayoweza kusababaisha watoto kupoteza maisha,” amesema.
Amewahakikishia wananchi kuwa nchi iko salama akisema amani na usalama ndiyo msingi wa ustawi wa kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.
Bashungwa amempongeza IGP Wambura, makamanda, maofisa na askari wa Jeshi hilo kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuendelea kulinda amani na utulivu ndani ya nchi, usalama wa raia na mali zao, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilivyoko ndani ya na nje ya wizara hiyo.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kupambana na uhalifu, huku jitihada kubwa zikielekezwa katika kushirikiana na wananchi raia wema katika kupata taarifa mapema ili kuzuia uhalifu kabla haujatokea.
“Watanzania wenzangu tukumbuke kinga ni bora kuliko tiba. Duniani kote Serikali za nchi huru na za kidemokrasia hutegemea Jeshi la Polisi katika ulinzi na usalama wa ndani ya nchi. Kwa kiasi kikubwa Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri ndiyo maana tunalala na kuamka huku usalama wa raia na mali zikiwa salama na amani na utulivu vikiendelea kuwa tunu yetu kuu,” amesema.
Amesema taasisi yoyote haikosi changamoto, hivyo hata ndani ya Jeshi la Polisi anakiri kuwa zipo.
“Kwa niaba ya Serikali, naomba kuwaahidi wananchi kwamba tunaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizi usiku na mchana bila kuchoka,” amesema.