Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ukaguzi na udhibiti wa rasimali za umma umechangia ukuaji wa uchumi kufikia wastani wa asilimia 7.4 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020.
Dk Mwinyi ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 18, 2024 katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Ukaguzi katika ukumbi wa Polisi Ziwani Zanzibar.
Amesema mafanikio ya kazi za ukaguzi wa rasilimali za umma, zimewezesha pia kuchochea kuimarika kwa utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, nishati ya umeme na huduma nyinginezo.
“Kazi za ukaguzi wa rasilimali fedha na rasilimali nyiginezo zimepelekea kuimarika kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo, masoko na mengineyo,” amesema Dk Mwinyi.
Kiongozi huyo, amesema mafanikio hayo yamechangiwa na udhibiti na ukaguzi bora wa rasilimali za umma, ambapo Serikali hupokea na kuzifanyia kazi hoja, ushauri na mapendekezo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti zake za kila mwaka.
“Kutokana na mafanikio haya, napenda kuchukua fursa hii kupongeza jitihada zinazochukuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kuimarisha utawala bora nchini wenye kuzingatia uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma,” alisema.
Amebainisha kuwa jitihada za taasisi hiyo zina mchango mkubwa katika kusukuma mbele fursa za maendeleo.
Dk Mwinyi amesema suala la kuimarisha utawala bora ni jambo la msingi katika kuleta maendeleo ya nchi, hivyo lazima kila mmoja kuongeza juhudi, uzalendo na uadilifu katika kuitumikia nchi.
Hata hivyo, amesema Serikali itaendelea na juhudi zake za kuijengea mazingira mazuri ofisi hiyo ili iweze kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa na kwenda sambamba na mabadiliko ya mara kwa mara ya ukaguzi duniani.
Sambamba na hayo amesema wajibu wa kuimarisha utawala bora katika matumizi ya rasilimali za umma si wa Serikali na ofisi ya CAG pekee bali ni la watu wote likijumuisha jumuiya za kimataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, viongozi wa dini, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, Serikali pamoja na makundi hayo yote kwa umoja wao yana mchango mkubwa katika kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma nchini.
Rais Mwinyi alipongeza ushirikiano uliopo baina ya ofisi ya CAG na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania katika kufanikisha kazi za ukaguzi wa hesabu za Serikali nchini kwani ushirikiano ni ishara ya kuendelea kuimarisha Muungano wa nchi.
Awali, akimkaribisha Rais Mwinyi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema ofisi hiyo ina mabadiliko makubwa yanayotokana na kusimamiwa vizuri na bodi ya ushauri.
Amewasisitiza wale waliopatiwa majukumu basi kuyasimamia vizuri ili lengo la kuwepo kwa ofisi hiyo liweze kufikiwa.
Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar Dk Othman Abbas Ali amesema utaratibu wa kusomwa kwa taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali hadharani na kujadiliwa kwa kina na uwazi katika Baraza la Wawakilishi kumeleta mafanikio makubwa yenye kujenga uelewa kwa wananchi juu ya matumizi ya fedha za umma.
Akiyataja mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushauri unaofanyiwa kazi na serikali unaotokana na ripoti za CAG kuhusu uanzishwaji wa mifumo ya kifedha serikalini limeleta tija kwa kuokoa fedha za Serikali kwa wastani wa asilimia 90.
Amebainisha kuwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi kwa wastani wa asilimia 96.8, kuongezeka kwa uelewa wa usimamizi wa fedha za umma kwa wastani wa asilimia 98 na matumizi ya mifumo kwenye shughuli za Serikali yameongezeka kutoka asilimia 48 hadi kufikia wastani wa asilimia 97.4
Amesema maadhimisho ya siku ya ukaguzi ni fursa kwa taasisi za umma kuwatumia wataalamu wao kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kukabiliana na vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.