Baraza la Madiwani Moshi lasitisha tozo za vibali vya sherehe ndogondogo

Moshi. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi limesitisha kwa muda utozaji wa vibali mbalimbali vya sherehe ndogo ndogo kama kumbukumbu za kuzaliwa, kipaimara, ubarikio na vikao vya kifamilia vinavyofanyika katika maeneo ya wazi au kumbi za sherehe.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Moris Makoi ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 18, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kusikiliza maoni ya wananchi na kugundua kuwa suala hilo ni geni kwao.

“Leo tumeamua kusitisha kwa muda matumizi ya Sheria Na. 39 ya mwaka 2024 pamoja na tangazo lake la Novemba 19, 2024, ili kutoa elimu kwa wananchi kabla ya sheria hiyo kuanza kutumika rasmi,” amesema Makoi. Amesema wamesikiliza maoni ya wananchi wengi na wamebaini kuna umuhimu wa kuhakikisha sheria hiyo haiwi mzigo kwao.

“Kazi yetu ni kuwahudumia wananchi kwa kuwasaidia kupata unafuu wa maisha, si kuwaumiza,” amesema mwenyekiti huyo.

Amefafanua kwa sasa wamesimamisha kutoza ada kwa sherehe ndogondogo, zikiwamo za Sh50,000 kwa washereheshaji (MC), Sh10,000 kwa wapamba ukumbi, Sh10,000 kwa wanaosambaza vyakula na vinywaji na Sh10,000 kwa wacheza muziki.

Amesema halmashauri itaendelea kuhakikisha sheria na huduma zinazotolewa kwa wananchi ni rafiki na zisizo kandamizi huku akisisitiza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuweka mazingira bora kwa wananchi.

“Kama alivyoelekeza Rais wetu, tunapaswa kuhakikisha sheria tunazopitisha zinaleta manufaa kwa wananchi na hazikandamizi. Hili ndilo jukumu letu,” amesema Makoi.

Mmoja wa wakazi wa wilaya hiyo, Amadea Chuwa amesema utekelezaji wa sheria ungeweza kuwa mzigo kwa wananchi endapo hawatapewa elimu ya kutosha.

“Hatupingani na sheria zinazowekwa, lakini ni muhimu wananchi wakapewa elimu kabla hazijaanza kutumika ili kuepusha migogoro kati ya serikali na wananchi,” amesema Amadea.

Related Posts