Wadau: Fedha za Samia Infrastructure Bond zisaidie kutatua kero za barabara

Mbeya. Jumla ya Sh90 bilioni zinatarajiwa kukusanywa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupitia mpango wa Samia Infrastructure Bond, huku wananchi wakiomba fedha hizo zielekezwe kumaliza changamoto za miundombinu ya barabara.

Hata hivyo, wananchi hao wamesifia mpango huo wakisema ushiriki wa wadau na wananchi katika kununua hatifungani utaongeza kasi ya kuboresha barabara, kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa taifa kwa ujumla.

Wakizungumza leo Jumatano Desemba 18, 2024 wakati wa kampeni ya Samia Infrastructure Bond jijini Mbeya, baadhi ya wadau wametoa maoni yao kuhusu matumizi bora ya fedha hizo.

Nahdel Dadkarim, mmoja wa wadau hao amesema mpango huu unapaswa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora. “Tuipongeze Serikali kwa ubunifu huu, lakini ni muhimu fedha zinazokusanywa zitumike ipasavyo. Kwa mfano, barabara nyingi za Jiji la Mbeya zinahitaji maboresho makubwa,” amesema Dadkarim, ambaye amechangia Sh100 milioni.

Naye Charles Daniel amesema kuna changamoto ya barabara kutokidhi viwango licha ya fedha kutengwa.

“Zipo barabara ambazo baada ya muda mfupi huanza kuharibika. Tunahitaji fedha hizi ziwe chachu ya mabadiliko ya kweli,” amesema.

Kwa upande wake, Sheikh Ibrahim Bombo ameshauri wale wanaoshiriki katika mpango huo wapewe motisha, kama kusamehewa baadhi ya kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Hawa wanapaswa kutambuliwa kama wadau wa maendeleo na hatua kama hizi zitawahamasisha wengi zaidi kushiriki,” amesema.

Meneja wa Benki ya CRDB Nyanda za Juu Kusini, Jenipher Tondi amesema lengo ni kukusanya Sh90 bilioni kupitia wananchi mmoja mmoja, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa ni Sh500, 000.

Amesema fedha hizo zitaelekezwa Tarura ili kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Ileje, Lugano Mwambingu kwa upande wake amesema mpango huo unalenga kuwa suluhisho kwa changamoto za fedha zilizokuwa zikiathiri utekelezaji wa miradi ya barabara.

Akizungumza katika kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameutaja mpango huo kuwa ni fursa ya kiuchumi kwa wananchi na wadau huku akihimiza uzalendo katika kuunga mkono juhudi za Serikali.

“Miundombinu bora itaondoa umasikini, na uchumi utaimarika. Ni jukumu letu kushiriki katika kuijenga nchi yetu, kama walivyofanya Ethiopia,” amesema mkuu huyo wa mkoa ambaye amechangia Sh200 milioni.

Related Posts