Mambo matatu kuwakutanisha Chadema Dar kesho

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inatarajia kukutana kesho Jumamosi Mei 11, 2024 katika ofisi yao kuu ya Mikocheni jijini Dar es Salaam.

 Hayo yamebainishwa jana Alhamisi Mei 9, 2024 kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya Chadema, John Mrema.

Kamati hiyo inakutana kujadili mambo makuu matatu ikiwamo,kupokea taarifa ya uchaguzi katika ngazi mbalimbali za chama, kupokea taarifa ya tathimini ya maandamano ya awamu ya kwanza ya mikoa katika wiki ya maandamano na kuweka mwelekeo wa awamu ya pili ya maandamano.

Pamoja na kufanya usaili na kuteua wagombea wa nafasi za uongozi katika kanda nne za Nyasa, Serengeti, Victoria na Magharibi.

Uchaguzi wa kanda hizo nne za awali, umekuwa na mvutano, hususan Kanda ya Nyasa na kuna wagombea wawili maarufu wanaochuana ambao ni mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Mchungaji Peter Msigwa, anayetetea nafasi hiyo kwa muhula wa tatu.

Mvutano baina ya vigogo hao ulikolezwa na kauli ya Lissu, ambaye alikwenda kushiriki maandamano na mkutano wa hadhara mkoani Iringa, vyanzo vya ndani vya chama hicho, vinaeleza ni mkutano ambao haukupaswa kufanyika.

“Kamati kuu ilizuia maandamano na mikutano Kanda ya Nyasa kwa sababu ya joto la uchaguzi.  Walifikia uamuzi huo kwa kuona kama yakifanyika yanaweza kuleta mpasuko. Sasa sijajua Lissu kwa nini alikwenda na hili limeleta shida sana,” amesema mmoja wa makada wa Chadema.

“Amekwenda kimakosa, ameongea hayo ya fedha chafu, chama kinatukanwa, yeye mwenyewe kwa nafasi yake ni mwenyekiti wa kamati ya maadili, hafu anakwenda kutoa tuhuma huko nje, yaani ni shida sana.”

Related Posts