WINGA wa Singida Black Stars, Victorien Adebayor kwa namna alivyoifuatilia Ligi Kuu Bara, amesema ameuona ushindani ambao mchezaji anayejituma unamjengea heshima mbele ya wadau wa soka.
Adebayor alijiunga na timu hiyo akitokea AS GNN ya kwao Niger aliyojiunga nayo Januari mwaka huu kwa mkopo kutoka Amazulu FC ya Afrika Kusini.
Mechi yake ya kwanza Adebayor aliingia kipindi cha pili dhidi ya Tanzania Prisons, timu hiyo ikishinda mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Sokoine, Desemba 16 wafungaji wa mabao hayo ni Marouf Tchakei na Kennedy Juma. Alipoulizwa aliionaje mechi yake ya kwanza? Alijibu; “Ni kawaida kwani nimecheza michuano tofauti, ambayo imenijenga kujiamini na uzoefu wa kipi napaswa kukifanya ninapokuwa uwanjani. Nilichokipenda ligi inahitaji kujitoa kulingana na ushindani wa timu pinzani ulivyo, kwa kifupi ni ligi nzuri na ngumu inayofanya mchezaji ajitume zaidi.”
Kuhusiana na ukimya wake baada ya kujiunga na timu hiyo, alisema; “Ni kweli watu wana haki ya kutaka kufahamu, ila yalikuwa mambo ya kawaida, jambo la msingi kwangu naangalia nini nitafanya kinachostahili kwa wakati huu.”
Adebayor aliyewahi kuhusishwa na Simba, alisajiliwa na Singida katika dirisha kubwa, lakini hakucheza mechi yeyote hadi hiyo dhidi ya Prisons.