Dar es Salaam. Matumaini na imani ya wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), yamebaki vile vile kama ilivyokuwa miaka 25 iliyopita, baada ya kumchagua tena Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wao taifa.
Profesa Lipumba anaukwaa wadhifa huo, baada ya kupata kura 216 katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho, akiwashinda wenzake saba waliokuwa wakichuana katika nafasi hiyo.
Hii inampa nafasi mwanasiasa huyo aliyebobea katika masuala ya uchumi ya kukiongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo na hivyo kuweka historia ya kuwa Mwenyekiti wa chama cha siasa kwa miaka 30 nchini.
Katika uchaguzi huo, uliofanyika jana Jumatano, Desemba 18, 2024, Profesa Lipumba ameshinda kwa kura 216 kati ya kura 592 halali zilizopigwa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Mashaka Ngole, anayemfuatia Profesa Lipumba ni Hamad Masoud aliyepata kura 181.
Aliyekuwa Makamu mwenyekiti wa CUF bara, Maftah Nachuma ndiye aliyefuatia akipata kura 102, huku Wilfred Rwakatare akipata 78.
Kisha alifuata Juma Nkumbi aliyepata kura sita, Athumani Kanali kura tano, Chifu Yema na Nkunyuntila Chiwale wakiambulia kura mbili kila mmoja.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, Othman Dunga ameibuka mshindi akipata kura 182 kati ya 533 halali zilizopigwa.
Dunga alifuatiwa na Miraji Mtibwiliko aliyepata kura 159, Magdalena Sakaya kura 140, Juma Nkumbi 34, Mohamed Ngulangwa 29 huku Komein Rwihura akipata kura 18.
Jumla ya kura 542 zilipigwa katika uchaguzi huo, huku 533 zikiwa halali na tisa ziliharibika.
Ngole ametangaza pia matokeo ya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti Zanzibar uliokuwa na wagombea watano.
Katika nafasi hiyo, Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 159 ndiye aliyeibuka mshindi, huku Husna Mohamed Abdallah akifuatia kwa kupata kura 150.
Aliyefuata ni Haroub Mohamed Shamis aliyepata kura 117, kisha Ali Rashid Ali kura 74 na Mohamed Habibu Mnyaa akipata kura 56.
Katika uchaguzi huo, kura saba ziliharibika kati ya 563 zilizopigwa.
Baada ya matokeo hayo, Ngole amesema uchaguzi wa ngazi ya wajumbe wa Baraza la Uongozi utafanyika leo asubuhi.