Ni muda wa kupanga, kuanza safari ya 2025

Wakati mwaka mpya unapokaribia, wananchi wanapaswa kufikiria mbinu za kuboresha hali zao ya kiuchumi, huku wakijifunza kutokana changamoto za mwaka uliopita.

Kupitia bajeti nzuri, kuwekeza, kupunguza madeni na kupata elimu ya kifedha, kila mmoja anaweza kuanza mwaka mpya kwa mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa wataalamu, Desemba ni kipindi cha sherehe na furaha, lakini pia ni wakati wa kujiandaa kwa mwaka mpya kwa umakini.

Familia na watu binafsi wanapaswa kuchukua tahadhari za kifedha, kuhakikisha wanakidhi mahitaji yao ya msingi na kupanga vizuri malengo yao ya mwaka mpya.

Wakati mwaka 2025 ukisubiriwa kwa hamu, ni wazi kwamba mipango thabiti ya kiuchumi itakuwa msingi wa mafanikio, hivyo Desemba ni zaidi ya sherehe, ni muda wa kutafakari, kujifunza, na kupanga maisha ya baadaye.

Kwa upande wa wafanyabiashara ni kipindi cha mavuno, lakini kwa watumiaji, ni wakati wa matumizi makubwa ambayo yanaweza kuathiri mipango ya kifedha ya Januari.

Biashara nyingi huongezeka bei za bidhaa kutokana na mahitaji makubwa, vyakula, nguo na vifaa vya mapambo na shule huonekana kupanda bei zaidi, hali hii huwafanya wengi kutumia zaidi ya wanavyopanga.

Wakati wananchi wakijiandaa kwa mwaka 2025, kuna umuhimu wa kuangalia jinsi ya kuimarisha uchumi wa familia na taifa kwa jumla. Wataalamu wanashauri kuweka malengo yanayotekelezeka na kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi.
 

Wachumi wanasisitiza kupanga bajeti kwa uangalifu na kuwekeza katika miradi midogo midogo yenye uwezo wa kuzalisha kipato kwa muda mrefu ili kuimarisha hali ya kifedha, hasa katika kipindi cha mpito kati ya mwaka mmoja na mwingine.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Jane Prosper anasema jamii zinapaswa kufikiria njia za kuendeleza mitaji yao badala ya kutumia fedha nyingi kwenye sherehe za Desemba.

“Huu ni wakati wa kuwekeza kwenye maarifa ya ujasiriamali na teknolojia. Biashara ndogo zinazotumia mtandao, kama vile uuzaji wa bidhaa za asili, zinaweza kuongeza kipato kwa gharama nafuu,” anasema.

Anasema kwa wale wenye vikundi ni kipindi muhimu cha kujitathimini nini cha kufanya kuelekea mwaka 2025, ambapo watu wanafikiria Januari ni mwezi wa mateso kwa sababu ya kutumia pesa nyingi kwa mwezi mmoja.

“Badala ya kutumia fedha nyingi kwa sherehe, unaweza kuwekeza katika biashara ndogo ambayo itakusaidia Januari na miezi mingine ya mwaka.”
Kwa mujibu wa wachumi, uamuzi wa kuwekeza sehemu ya mapato kwenye miradi yenye tija ni muhimu katika kujenga maisha bora, hasa wakati wa changamoto za kiuchumi zinazoendelea kuathiri kaya nyingi.

“Uwekezaji mdogo unachangia siyo tu katika kupunguza utegemezi wa ajira za kawaida, bali pia huimarisha usalama wa kifedha wa familia kwa miaka mingi ijayo,” walihitimisha.
 

Kujifunza kutoka mwaka uliopita

Jane anashauri watu kutafakari jinsi walivyotumia kipato chao mwaka 2024 na kubaini maeneo ya kuboresha.

“Wengi wanaweza wakawa walitumia pesa zao kwenye matumizi yasiyo ya lazima, hivyo ni wakati sasa wa kuweka vipaumbele. Muhimu kuangalia makosa ya kifedha yaliyofanywa mwaka uliopita na kuhakikisha hayarudiwi,” anasema.
Anasema familia nyingi zinatumia fedha kiholela bila kujua zinapotea wapi, anza mwaka kwa kupanga bajeti kulingana na kipato chako halisi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama sherehe za gharama kubwa au ununuzi wa vitu visivyo na umuhimu.

Katika hilo, ameweka mkazo wa kutazamwa kwa maeneo yaliyoshindikana mwaka 2024 kupangwa na kuboresha mwaka ujao, hii inahusisha kufuatilia matumizi na kuacha tabia za kifedha zisizo na tija.
 

Mchumi mwingine, Lucas Mvungi anasema kwamba mwaka mpya ni fursa ya kuanza tabia za kifedha bora, kama kuwekeza kwenye miradi midogo au kuweka akiba.

“Watu wanatakiwa kuwekeza katika maeneo ambayo yana uhakika wa faida, kama ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga, au hata biashara ya mtandaoni. Ukishindwa kuwekeza, hakikisha una akiba ya dharura inayoweza kukufikisha miezi sita,” anasema Mvungi.

Anasema watu wanapaswa kuzingatia uwekaji kuliko ukopaji, hususani mikopo umiza na yenye riba kubwa. “Usikubali madeni yakutawale, ikiwa unalazimika kukopa, hakikisha lengo ni kukuza mtaji,” anasema.

Hata hivyo, Mvungi anasema kwa wale wenye vikundi vya kuweka pesa na kukopeshana kuna haja ya kupata elimu ya kifedha tena ili kujua kuwa malengo yao waliyokusudia kama wameyafikia na kama la walikosea wapi.

“Serikali na taasisi binafsi zinapaswa kutoa mafunzo ya kifedha kwa wananchi. Hii itawasaidia kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, uwekezaji na matumizi mazuri ya fedha,” anasema.
 

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi wameonyesha wasiwasi kuhusu madeni yanayowakabili kwa mwaka wa 2024 ambapo wanajikuta wanageuza nayo mwaka unaofuata.

Moses Simon, mfanyabiashara wa Kariakoo, anasema: “Mwaka huu umekuwa mgumu kwangu kwa sababu ya riba kubwa za mikopo. Lengo langu mwaka mpya ni kulipa madeni haraka na kuepuka kuchukua mikopo isiyo ya lazima.”
Hali hii inaungwa mkono na mkazi wa Tandika, Amina Kassim, ambaye anasema amejifunza umuhimu wa kuweka akiba baada ya kuishi kwa mkopo, mwaka huu ulimfanya kukosa amani.
“Mwaka huu mpya, nitalenga kuweka angalau asilimia 10 ya kipato changu kwenye akiba, nilikuwa nakonda kwa sababu ya madeni, kila siku kipato ninachokipata nilikuwa narejesha marejesho tu,” anasema Amina.
 

Kwa mujibu wa Hassan Said, mchambuzi wa masoko, mwaka mpya huleta fursa nyingi za kiuchumi ambazo watu wanapaswa kuzitumia.

“Uwekezaji katika sekta kama teknolojia, kilimo na usafirishaji una nafasi kubwa ya kuleta faida. Hata hivyo, wananchi wanapaswa kufanya utafiti kabla ya kuwekeza,” anasema.
Anasema kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi wanaamini kwamba kujiingiza kwenye biashara ndogondogo ni njia rahisi ya kuanza safari ya kiuchumi.

“Unaweza kuwakuta wakijadili kuhusu kuanza biashara mwakani, lakini hajafanyia utafiti, hivyo anajikuta kwenye majuto ya kupoteza pesa zake kwa sababu alimuona mwenzie anafanya au alimshauri.”

Related Posts