MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amewataka wenye viti wote wa serikali za mitaa wilayani humo kuto kuchongesha mihuri na kuitumia katika kuwahudumia wananchi mpaka pale Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itakapotoa mwongozo .
Amesema halmashauri hiyo ya jiji ndiyo itakayo toa mihuri itakayotumika katika ofisi hizo hivyo ni kosa kwa mwenyekiti kuchonga mhuri bila ridhaa ya serikali na kuitumia.
Aliyasema hayo alipokuwa akifunga semina ya kuwajengea uelewa wenye viti wapya wa mitaa 159 ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mpogolo alisema, mhuri ni nyaraka ya serikali hivyo serikali ndiyo yenye mamlaka ya kuiandaa na kuikabidhi kwa watumishi wake kwaajili ya kuwahudumia wananchi.
“Ninawaomba ambao wamechonga ile mihuri wairudishe waifungia wasiitumie. Tupate mwongozo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , tupate mwongozo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa ambaye ataleta maelekezo,”alieleza Mpogolo.
Alisema mihuri itaanza kutumiwa na wenyeviti wa serikali za mitaa mpaka pale watakapopewa miongozo na mamlaka husika na siyo vinginevyo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wenye viti hao kuendelea kuwahudumia wananchi kikamilifu na kuimarisha uhusiano.
“Naomba tusichomoke nje ya sheria. Tuache matamanio tufuate maelekezo. Kama kuna barua unaandika nenda kaiandike halafu mpelekee Ofisi Mtendaji agonge muhuri,”alieleza.
Aliwakumbusha wenye viti hao barua zote wanazo idhinisha na kugonga mihuri nyingi zina kwenda katika ofisi za serikali hivyo wajihadhari na matumizi ya mihuri iliyo kinyume cha utaratibu.
“Tuvute subira muda siyo mrefu tutapata maelekezo na tutaishi katika maelekezo. Ni wajibu wangu kuwalinda nyie.Mstamani kufanya jambo litakalo wapeleka katika kifungo,”alieleza.
Pia Mpogolo , aliwataka wenye viti hao kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya serikali, miradi inayo tekelezwa katika maeneo yao na kuimarisha uhusiano wao na serikali.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani, aliwataka wenye viti hao kuwa kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi na kutambua ni wakati gani wanakuwa upande wa wananchi na wakati gani wanakuwa upande wa serikali.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mustafa, Kata ya Pugu, Fikiri Rajabu ‘Timbwa’ alisema semina hiyo imewapa mwanga wa uongozi na namna bora ya kuwatumikia wananchi.
“Tumepata semina ya siku tatu. Juzi tulikutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ngazi ya mkoa juzi na jana tulianza semina ngazi ya wilaya. Semina zimetupa maelekezo mazuri, tumejijenga kutumikia wananchi, kuwa rafiki na kiungo muhimu baina ya na serikali na wananchi katika mitaa yetu,”alisema Timbwa.