Ulega ataka kasi ya kijeshi ujenzi miradi ya dharura ya barabara

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi ya dharura inayotekelezwa.

Ulega ametoa maagizo hayo kwenye mkutano uliohusisha menejimenti na mameneja wa Tanroads wa mikoa yote nchini, uliofanyika mjini Dodoma Desemba 18, 2024.

Amesema miradi ya dharura inapaswa kushughulikiwa kidharura.

“Fanyeni kazi kwa kasi usiku na mchana hususani kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa,” amesema.

Ulega amesema Tanroads wanatakiwa kwenda kwa kasi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na Serikali.

Amesema kuna mvua zinakuja zinazoweza kusababisha maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.

Ulega amesema barabara zilizoharibika kutokana na mvua za masika na za El-Nino zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi, hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka.

Mkutano huo ni wa kwanza kati ya viongozi wa Tanroads na Ulega tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ulega aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi kabla ya uteuzi wa Rais wa Desemba 8, 2024 amewapongeza wafanyakazi wa Tanroads kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, Tanroads imekamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,198 kwa kiwango cha lami.

Amewataka mameneja kufanya kazi kwa kujiamini na weledi ili kuleta tija na ufanisi katika sekta ya ujenzi nchini, pia kuondoa kero ya miundombinu mibovu kwa wananchi, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Ulega ametoa rai kwa mameneja wa mikoa kuhakikisha maeneo yote yenye msongamamo wa magari, hususan kwenye majiji na manispaa yanafanyiwa usanifu yakinifu kwa ufasaha kulingana na mahitaji ya sasa na miaka mingi ijayo.

Ameagiza kuratibiwa vizuri ili kupunguza msongamano na kuwawezesha wananchi kufanya kazi kwa wakati.

Hata hivyo, amewahakikishia mameneja kuwa Serikali itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto za wakandarasi ili wafanye kazi zao kwa kasi kuendana na malengo ya Serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Aisha Amour amesema Tanroads itaendelea kuhakikisha barabara kuu za mikoa na madaraja yanajengwa ili kupitika wakati wote wa mwaka.

Amewataka mameneja wa Tanroads kuboresha usimamizi wa miradi, kulinda hifadhi za barabara na kupendezesha miji kwa taa za barabarani na utunzaji wa mazingira pembezoni mwa barabara.

Related Posts