Lipumba ambaye anaweka rekodi kwa kuwa mwenyikiti wa sasa kwa kipindi kirefu zaidi anakabiliwa na jukumu la kurejesha ushawishi wa chama hicho wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu hapo mwakani.
Ni tambo na vijembe ambavyo mara nyingi Profesa Lipumba amekuwa akivihanikiza wakati anapopanda katika majukwaa ya kisaasa vikielelezwa kwa chama tawala CCM na sera zake.
Soma pia: Lipumba aitaka serikali kuionya Urusi kuhusu kundi la Wagner
Mwanasiasa huyo ambaye amepata kugombea nafasi ya urais zaidi ya mara tatu, amechaguliwa kuongoza tena chama hicho cha upinzani katika mkutano mkuu uliomalizika jana usiku, akiwashinda wapinzani wake kwa idadi ndogo ya kura. Matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa chama hicho Mashaka Ngole, yalionyesha kuwa Lipumba ametetea nafasi yake kwa kuondoka na kura 216, wakati aliyemfuatia Hamad Masoud akijikusanyia jumla ya kura 181.
Ushindi wake mwembamba dhidi ya aliyekuwa makamu wake uanashiria namna mwanasiasa huyo anavyokabiliwa na mtihani wa kimahesabu ndani ya chama na kwamba huenda atalazimika kuzikagua upya sera zake kelekea katika kipindi chake cha miaka mitano ijayo.
Soma pia: CUF yapinga vikali kuibuka kwa pendekezo jipya kuhusu katiba
Lipumba anaendelea kusalia katika uongozi wa chama katika wakati ambapo ushawishi wa chama hicho ukiendelea kuporomoko na kuzua wasiwasi juu ya majaliwa ya chama chenyewe wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani.
Cuf ambayo miongo kadhaa iliyopita ilizitawala siasa za upinzani kuanzia visiwani Zanzibar mpaka bara, sasa siyo tishio tena katika medani za siasa, na kulingana na baadhi ya wachambuzi wa mambo kiongozi huyo inaweza ikawa ni sehemu ya sababu ya kuanguka kwa chama hicho.
Mwandishi wa habari wa siku nyingi na ambaye pia wakati mmoja amewahi kuwa mbunge, Said Kubenea anasema Lipumba hakupaswa kugombea tena katika kinyang’anyiro hicho na kwamba haiba yake ilidorora tangu alipokikacha chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baadaye kuamua kurejea tena.
Hata hivyo, chama hicho bado kimebakiza ushawishi wake katika baadhi ya maeneo ikiwamo maeneo ya pwani ya kusini. Wakati baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa katika mchaka mchaka wa uchaguzi wa ndani vikijipanga kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Chama kingine cha upinzani Chadema kinatarajiwa kufanya uchaguzi wake Januari 22 huku macho ya wafuatiliaji wa mambo yakiekekezwa kujua nani atakuwa kinara wa chama katika nafasi ya uenyekiti.