Yanga, Mashujaa pointi tatu ngumu

Hakuna timu inayoweza kuvuna pointi tatu kirahisi wakati Yanga itakapoikaribisha Mashujaa FC leo katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge kuanzia saa 10:00 jion

Timu zote mbili zimeonyesha kuwa na safu za ulinzi ambazo hazifungiki kirahisi jambo ambalo linalazimisha kila upande kuhakikisha unakuwa na mipango mizuri ya kushambulia ili iweze kupata pointi tatu leo.

Yanga katika mechi 11 ilizocheza imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne huku Mashujaa katika mechi 14 ikifungwa mabao nane ikiwa na wastani wa kufungwa bao 0.6 kwa mechi.

Huo ni mchezo wa 12 kwa Yanga katika ligi hiyo msimu huu ambapo inapambana kutetea taji lake kwani hivi sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 27.

Mashujaa iliyopo nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na pointi 19, mchezo wa leo inahitaji kushinda ili kuweka hesabu sawa za mzunguko wa kwanza kwani ndiyo wa mwisho kwao kabla ya kuingia mzunguko wa pili ambao nao utakuwa na mechi 15.

Yanga na Mashujaa huu utakuwa ni mchezo wa tatu katika ligi kukutana huku mechi mbili za msimu uliopita Yanga ikishinda zote.

Mbali na rekodi hiyo nzuri kwa Yanga, lakini timu hiyo haikupata ushindi mechi mbili kati ya tano za mwisho katika ligi ikifungwa 3-1 dhidi ya Tabora United na 1-0 dhidi ya Azam, huku ikizifunga Namungo 2-0, Singida Black Stars (1-0) na Coastal Union (1-0).

Kwa upande wa Mashujaa, ni timu ambayo haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo za mwisho ikiambulia sare zote huku mbili kati ya hizo ikishindwa kufunga bao lolote.

Uwepo wa David Ulomi na Ismail Mgunda, kunaifanya Mashujaa kuwa si timu ya kuibeza katika kucheka na nyavu kwani nyota hao ndiyo wanawabeba zaidi, hadi sasa kila mmoja amefunga mabao mawili huku Mgunda akiwa pia na pasi tatu za mwisho ikimfanya ahusike kwenye mabao manne peke yake.

Yanga iliyotoka kucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika, inarejea kwenye ligi ikiwa bila ya huduma za wachezaji wake kadhaa ambao ni majeruhi akiwemo Djigui Diarra, Clatous Chama, Maxi Nzengeli na Kennedy Musonda.

Kukosekana kwa wachezaji hao ambao wamekuwa muhimu zaidi kikosi cha kwanza, kutaifanya Yanga kuwa na mabadiliko makubwa na kutoa fursa kwa wengine kuchukua nafasi zao.

Hata hivyo, Kocha wa kikosi hicho, Sead Ramovic amesema atawatumia nyota waliopo tayari kwa ajili ya kufanya vizuri.

Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema: “Tumeshamaliza mechi tatu za Ligi ya Mabingwa na sasa akili yetu inaelekea kwenye Ligi Kuu. Tunataka kupambana kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, nimezungumza na wachezaji umuhimu wa pointi tatu za mchezo wa kesho (leo) na wako tayari kwa hilo.”

Mohamed Abdallah ‘Bares’ ambaye ni Kocha wa Mashujaa, alisema, “Tuna wachezaji kama wawili majeruhi lakini wanaendelea vizuri, waliopo wapo tayari kwa mchezo huu na tumeshawapa majukumu ya kufanya katika mchezo wa kesho (leo) kilichobaki ni kwao kwenda kutekeleza tulichowafundisha.”

Related Posts