Wakati mstaafu akijiandaa na kujipa moyo akisubiri nyongeza ya shilingi elfu hamsini aliyoongezwa kwenye pensheni yake ya ‘Laki si pesa’ baada ya miaka 20 na anayotegemea iingie mfukoni mwake mwishoni mwa ‘Njaanuari’, anafarijika kuona angalau jamii yake inamuunga mkono kwenye malalamiko yake kuhusu taabu zinazomkabili. Maoni hayo ya wananchi anayasoma kwenye mitandao ya kijamii lakini hasa kwenye hii kona yetu ya kila Ijumaa ya wastaafu.
Jamii haijasema sana kuhusu nyongeza ya shilingi elfu hamsini kwenye ‘Laki si pesa’ yake ya miaka 20, labda kwa kuona mradi hatimaye amepata nyongeza basi aishukuru tu Siri-kali. Mstaafu anaishukuru Siri-kali kwa elfu hamsini hii. Huwezi kuiokota mahali. Mstaafu mwenyewe anaisaka kwa miaka 20 na hajaiokota mahali. Ikumbukwe tu kwamba ni Siri-kali hiihii iliyomfanya mstaafu huyu wa kima cha chini akae miaka 20 bila nyongeza ya pensheni.
Haya, mstaafu wetu anaishukuru Siri-kali na kibubu chake kwa nyongeza hiyo, ingawa hajajua sawasawa ni nani amemuongeza elfu hamsini yake. Hafahamu sawa-sawa ni nani kati ya Siri-kali na kibubu chake ndiyo imeamua kwamba nyongeza hiyo iingie mifukoni mwa wastaafu mwisho wa ‘Njaanuari’ na siyo hii Desemba ili apate nafasi ya kujipongeza na wanawe na wajukuu zake. Atalifanyia kazi.
Ndiyo, mstaafu wetu anashukuru kwa nyongeza hiyo pamoja na kwamba bado iko kwenye makaratasi. Anajiuliza mno kama kulikuwa na umuhimu gani wa kuitangaza nyongeza katikati ya Novemba lakini mpaka mwezi mmoja na nusu baadaye, mwishoni mwa Njaanuari ndiyo iwe mifukoni mwa wastaafu, hawahawa walioisubiri kwa miaka 20 ndiyo ipatikane, japo si kwa namna walivyotegemea.
Wastaafu wenyewe wa kima cha chini waliolianzisha Taifa hili na kulijenga kwa damu na jasho lao wamebaki wangapi, jamani? Hivi hesabu ya kuwaongeza elfu hamsini kwenye pensheni yao ni kubwa sana kiasi cha kuchukua miezi miwili na nusu, Novemba katikati hadi mwisho wa ‘Njaanuari’? Mngekuwa mnawaongeza shilingi laki mbili unusu ili pensheni iwe shilingi laki tatu unusu si nyongeza ingetoka miezi sita baadaye?
Mstaafu wetu kama walivyo wastaafu wengi wenzake wa kima cha chini, haijui Masters wala PhD ni vitu gani kwenye mahesabu, lakini anajua kuwa utashi wake tu ndiyo ungemuwezesha kufanya wastaafu waliopewa nyongeza ya pensheni katikati ya Novemba waipate mwezi huohuo mwishoni, hata umeme ukifanya vitu vyake vya kukata umeme kwenye kompyuta na kuchelewesha mambo, basi angalau wapate nyongeza yao mwezi mmoja baadaye, siyo miezi miwili na nusu baadaye.
Hawa ni wastaafu wa kima cha chini ambao wameishaisubiri nyongeza ya pensheni yao kwa miaka 20, mnawasubirisha miezi miwili na nusu tena ya nini ili kuipata? Ni dharura, si mngeitangaza mkiwa tayari? Hivi hesabu ya elfu hamsini jumlisha shilingi laki moja kwa wastaafu waliopo wasiozidi laki tano ni kubwa na ngumu kiasi hicho cha kuhitaji miezi miwili na nusu kuikamilisha?
Mstaafu haoni aibu kukiri kwamba nyongeza ya pensheni ya kialfu hamsini ingemsaidia sana mwezi huu, kuliko waheshimiwa wasivyojua. Miaka miwili nyuma aliendekeza shida zake na kuziweka kwenye mfuko wa rambo zionekane na kila mtu, ikiwemo hii benki ya dotcom ambayo ilichangamkia kumpa mkopo ambao riba yake inamfanya apate shilingi elfu arobaini na sita tu kwa mwezi badala ya ‘Laki si pesa’ yake.
Mstaafu wetu anajua kuwa waheshimiwa wangechangamka wangeweza kufanya aipate nyongeza ya pensheni mwezi uleule wa Novemba ilipotangazwa, kama ingechelewa basi angeipata Desemba ikamwezesha kupokea tena ‘Laki si pesa’ yake, japo kwa maumivu ya riba ya mkopo! Mara moja-moja wahusika mlioshiba wakumbukeni wastaafu wa kima cha chini wenye njaa kama huyu mstaafu wetu. Angalau ajidai kwa mwaka mmoja uliobaki ili mkopo na riba yake vichape lapa.
Ndiyo maana mstaafu wetu huwa anafarijika anaposoma kuhusu wanachoandika wanajamii kuhusu taabu zao. Yote yanaonyesha jamii kuguswa na yanayompata mstaafu na kutaka juhudi ifanyike kwa wahusika kumsaidia mstaafu wa kima cha chini wa taifa. Ni mengi kutoka kwa wengi. Kuna wanaotaka wastaafu kurudishiwa matibabu ya bure ili wayamudu maradhi yao ya kiutu uzima.
Wako pia wanaotaka wastaafu ambao wana utaalamu wa kazi zao na nguvu, japo kasi imepungua kidogo kwa utu uzima wao, wapewe ajira hata kwa mkataba ili ujuzi wao uweze kulisaidia Taifa wakishirikiana na vijana.
Wapo wanaopendekeza wastaafu kupewa kazi za kitaifa kama za kuandikisha na kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani ambao wanaweza kufanya kazi njema na walimu wakabaki shule kufundisha wanafunzi.
Mstaafu anafarijika mno kwa mawazo ya wanajamii wengi ambao wanaonyesha kuguswa na hali duni ya mstaafu wa kima cha chini wa Taifa hili. Anawashukuru sana wanajamii. Awakumbushe tu kuwa, sauti ya wengi ni sauti ya Mungu na Mungu ni mwema, atawasikia tu. Muwe na Krisimasi njema.