Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka idadi ya wagonjwa wa kipindupindu katika mikoa ya Mwanza na Simiyu, Marekani imetoa msaada wa ziada wa Sh1.18 bilioni (sawa na Dola 500,000) kwa mikoa hiyo.
Taarifa iliyotolewa leo Desemba 19, 2024 kwa vyombo vya habari na Ubalozi wa Marekani Tanzania imeeleza, mpango huo ni mwendelezo wa msaada wa afya wa Serikali ya Marekani kwa jamii zilizoathirika na milipuko ya kipindupindu nchini Tanzania.
Kupitia mradi wa majisafi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (Usaid), Marekani imetoa Sh591 milioni (Dola 250,000) kwa kila mkoa (Simiyu na Mwanza) na kutuma timu za kiufundi za maji, usafi wa mazingira na usafi wa mikono kusaidia ofisi za afya za mikoa husika.
Imeelezwa timu hizo kwa kushirikiana na wadau wazawa zinatoa vidonge vya kutakasa maji, kusafisha vyanzo vya maji na kuendesha programu za uhamasishaji wa jamii ili kuzuia kuenea kwa kipindupindu.
“Hatua yetu ya haraka inaonyesha dhamira yetu ya kuokoa maisha na kupunguza kuenea kwa kipindupindu Tanzania,” amesema Kaimu Balozi Andrew Lentz katika taarifa hiyo.
“Marekani itaendelea kuwa mshirika wa karibu katika kuimarisha mifumo ya afya ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kukuza upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira, mambo muhimu katika kupambana na ugonjwa huu unaoweza kuzuilika,” amesema.
Mapema mwaka huu, Marekani ilitoa Sh473 milioni (Dola 200,000) kwa ufadhili wa dharura kusaidia juhudi za kuzuia na kukabiliana na kipindupindu kutokana na milipuko iliyoathiri mikoa 18 ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu Septemba, 2023 wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka Tanzania ambapo zaidi ya 2,200 wameripotiwa kuugua huku, vifo vikitajwa kuwa zaidi ya 40.
Serikali ya Marekani, kupitia Usaid na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), imeendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa jamii za Tanzania kuongeza upatikanaji wa majisafi, kuwafundisha wafanyakazi wa afya ya jamii na wakazi kuhusu njia bora za kuzuia na kusaidia harakati za haraka za timu za kukabiliana na mlipuko.
Taarifa imesema CDC inatoa vidonge vya kutakasa maji kwa watu walio na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), na kuongoza juhudi za kudhibiti katika vituo vinavyofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (Pepfar).
Msaada huo wa ziada unaelezwa utaimarisha uratibu, kuchochea rasilimali na kuwezesha jamii zilizoathirika zaidi Simiyu na Mwanza kuzuia kuenea kwa kipindupindu na kuokoa maisha.
Msaada huo wa dharura wa Sh118.19 bilioni (Dola 50 milioni) ni sehemu ya ahadi ya Marekani ya kubadilisha miundombinu ya maji, usafi wa mazingira na usafi wa mikono nchini Tanzania. Hadi sasa, zaidi ya Watanzania 2000,000 wamepata majisafi na huduma bora za usafi wa mazingira.
“Marekani inaendelea kuunga mkono juhudi za kupanua upatikanaji wa majisafi na mifumo bora ya majitaka kama msingi wa maisha yenye afya na ustawi kwa Watanzania wote,” imeeleza taarifa hiyo.