Hofu yatanda wagonjwa wa kipindupindu wakifikia 46 Mbeya, chanzo chatajwa

Mbeya. Ugonjwa wa kipindupindu umeendelea kusambaa jijini Mbeya baada ya idadi ya wagonjwa kufikia 46, huku uhaba wa huduma ya maji ukitajwa kuwa sababu na kuleta hofu kwa wananchi wakiomba serikali kuingilia kati.

Desemba 11 idadi ya wagonjwa walikuwa 22 ambao walibainika katika kata nane, ambapo kwa sasa zimeongezeka kufikia 18 kati ya 32 za jiji hilo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 19, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Yesaya Mwasubila amethibitisha idadi hiyo kuongezeka akieleza kuwa tatizo kubwa ni uhaba wa maji.

Amesema pamoja na juhudi zinazoendelea kufanywa na kamati ya Afya ya Jiji kwa ukaribu na Mkuu wa Wilaya hiyo, Beno Malisa, lakini wamezidiwa kutokana na ukosefu wa maji.

“Watu hawana maji, muda mwingine yanatoka kwa mgawo inasababisha wengi wao kutumia maji ya visima ambavyo havina ubora madhara yake ni hayo,” alidokeza.

“Ongezeko hili linatishia sana na kuleta hofu, lazima tushirikiane na wadau na tumekuwa nao watu wa Bonde na Mamlaka ya Maji Mbeya kuona huduma inapatikanaje,” amesema Dk Mwasubila.

Ameeleza kuwa kamati ya afya inatarajia kuketi kufanya tathmini ikiwamo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuchukua tahadhari na kukagua visima na kuchukua hatua.

Amesema pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo, kutokana na mifereji ilivyo inasababisha maji kutuama katika maeneo tofauti ikiwamo kwenye visima ambavyo vimechimbwa kienyeji.

“Kata za Ilemi, Isanga na Iganzo visima ni vingi na havina ubora, mvua ikinyesha watu wanajaza kwenye visima anatumia kwa shughuli zake za nyumbani,” amesema Dk huyo na kuongeza.

“Nimeongea na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wanasema maji hayatoshi kwa hiyo tatizo kuisha itakuwa changamoto,” amesema.

Baadhi ya wananchi jijini hapa,  wamesema licha ya operesheni iliyofanyika chini ya Mganga Mkuu, matokeo yake hayawezi kuleta tija iwapo miundombinu ni mibovu.

Sakina Bahebe ambaye ni mchuuzi wa mbogamboga na matunda, amesema ugonjwa huo unasambaa kutokana na ukosefu wa maji na barabara za pembezoni kutokuwa safi.

“Tulishasema kuwepo na maji ya uhakika, wataalamu wametutembelea na kutueleza tuchukue hatua, lakini itakuwa ngumu kwa hali hii,” amesema Sakina.

Naye Bernard Mwampamba amesema Serikali iingilie kati kabla ya ugonjwa huo haujasimamisha shughuli za uchumi.

“Wizara ya Afya na Mamlaka ya Maji zichukue hatua haraka, wasiiachie halmashauri pekee kwa kuwa awali tulisikia watu 17, baadaye 22 leo idadi imepanda hadi 46, tunahofia kufunga shughuli,” amesema Mwampamba.

Related Posts