African Sports warejea Championship | Mwanaspoti

Tanga. TIMU za African Sports ‘Wanakimanumanu’ na Kiluvya zimefanikiwa kupanda Ligi ya Championship baada ya kutinga fainali ya First League (zamani Ligi Daraja la Pili), ambapo kesho, Jumamosi zitakutana kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ili kutafuta bingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Kiluvya imefika hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya kutoka suluhu na Malimao FC wakati African Sports waliichapa Mwadui mabao 2-1 kwenye mchezo wa nusu fainali michezo yote ikichezwa jana, Alhamisi kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

African Sports inarejea Championship baada kushuka daraja msimu uliopita ikishushwa na TMA kwa kufungwa mabao 4-1 ugenini kisha nyumbani kwenye uwanja wa Mkwakwani iambulia sare ya 1-1.

Msimu wa 2015/2016 ni kama vile ulikuwa na mkosi kwa Mkoa wa Tanga baada ya kushuhudia timu zake zote tatu zilizokuwa zikishiriki Ligi Kuu Bara yaani African Sports, Coastal Union na Mgambo zilishuka daraja kwa mpigo na kuwafanya mashabiki kushindwa kushuhudia burudani ya soka ya ligi hiyo kwa muda.

African Sports yenye maskani yake barabara ya 12 jijini Tanga ambao pia ni mabingwa wa Kombe la Muungano 1988 imepanda daraja msimu huu ikiwa imepoteza michezo miwili  pekee kwenye michuano ya First League.

Wakati fainali hiyo ya kumtafuta bingwa ikiwa inasubiriwa kwa hamu mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakuwa ni kati ya Mwadui FC dhidi ya Malimao FC katika uwanja huohuo.

Pamoja na fainali hiyo African Sports na Kiluvya tayari zimeshapanda daraja wakati Malimao FC na Mwadui zinalazimika kucheza mechi za mtoano zikisubiri timu kutoka Championship.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Klabu ya African Sports, Hamza Bwanga  amesema wanakwenda kufanya majaribio kwa vijana wote wanaochezea timu za ngazi ya wilaya na Mkoa wa Tanga ili kuendeleza mpango wao wa kukuza vipaji vya wazawa.

Bwanga amesema huo ni mpango wao wa muda mrefu ambao wamekuwa wakiutekeleza na umekuwa na tija, pia kinachokwenda kufanyika sasa ni kufikiria namna ya  kukiongezea nguvu kikosi ili kufanya vizuri msimu ujao kwenye Championship.

“Bado tunaendelea na mpango wetu wa Tanga kwanza. Tutakwenda kufanya majaribio  katika wilaya zote nane za Mkoa wa Tanga na ndio kipaumbele chetu kikubwa.  Tutatazama vijana wenye vipaji kwa muda mrefu, tumekuwa tukitumia njia hii na  imetusaidia na hata wachezaji ambao wamewezesha kuipandisha timu wengi ni wazawa,” amesema Bwanga.

Wakati mashabiki na wapenzi wa African Sports wakifurahia kupanda daraja, Bwanga amesema haikuwa rahisi kufikisha timu hapo ilipo kwani wamepitia katika vipindi vigumu ambavyo vilihitaji kujitoa zaidi vinginevyo wangeshindwa.

“Ilikuwa ni ngumu sana kwa sababu ligi hii ya daraja la pili (First League) mara nyingi kuwa na wadhamini ni ngumu. Tumesafirisha timu msimu mzima na kuiendesha kwa kuchangishana sisi wenyewe na kutegemea wadau, lakini sasa kikubwa ni kuangalia mbele sio tulikotoka,” amesema.

“Tunakwenda kwenye Championship ligi ambayo inaonyeshwa (kwenye runinga). Tunaamini wadhamini na wadau watajitokeza kutushika mkono kwa hali na mali. Tunaahidi kwenda kufanya usajili wa wachezaji ambao watatufanya tupande Ligi Kuu. Sisi hatutaki kushiriki (Championship) ila itakuwa ni njia ya kupita tu kuelekea Ligi Kuu.” 

Related Posts