Dar City imejipanga | Mwanaspoti

DAR City kwa sasa ndiyo habari ya mjini kwenye mchezo wa mpira wa kikapu na katika kuhakikisha inazidi kuimarika, kimya kimya imeshusha majembe wapya kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano itakayoshiriki.

City ambao ni mabingwa wa Ligi ya Kikapu ya Taifa (NBL), iliwasajili wachezaji hao mapema na tayari wameshaichezea kwenye michuano ya Afrika Mashariki.

Wachezaji hao ambao walitamba kwenye Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (BDL)ni Stanley Mtunguja (Ukonga Kings), Amin Mkosa (Mchenga Star), Fotius Ngaiza (Vijana City Bulls),  Mwalimu Heri na Evance Davies (UDSM Outsiders).

City iliwasajili nyota hao kutokana na uwezo wao na walianza kutumika katika mashindano ya Ligi ya Taifa (NBL), yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chinangali, Dodoma.

Mmoja wa nyota waliosajiliwa, Davies anayecheza namba 1 ‘point guard’, aliisaidia UDSM kucheza   fainali ya ligi ya BDL.

Akizungumzia usajili huo, Kocha wa timu za vijana wadogo, Ally Issa kutoka Kinondoni alisema bosi wa timu hiyo amefanya uwekezaji mkubwa utakaowasaidia kuwa bora mwakani.

“Kwa kweli uwekezaji aliofanya Mussa Mzenji kwa timu hiyo, naamini mwakani timu hiyo itakuwa timu  bora,” alisema Issa.

Related Posts