Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mfanyabiashara Daisle Ulomi, aliyefariki dunia kwa ajali umefikishwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Madale Betheli kwa ibada ya kuagwa.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Ulomi aliyekuwa anafanya biashara ya fedha kupitia mitandao ya simu alipata ajali Desemba 11, 2024 saa 7:55 mchana eneo la Gereji. Mwili wake ulitambuliwa na familia Desemba 16, 2024 katika mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, siku tano tangu alipotoweka.
Awali, familia ilitoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa Ulomi akitoka ofisini kwake Sinza Kijiweni, Dar es Salaam.
Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema Ulomi aliyekuwa kwenye usafiri wa pikipiki aina ya Boxer, aligonga lori la mizigo kwa nyuma katika Barabara ya Mandela.
Mwili wa Ulomi umefikishwa kanisani saa 7:46 mchana ukitokea nyumbani kwake Mikocheni, Mtaa wa Manyara.
Baada ya kuhitimishwa ibada iliyohudhuriwa na familia, ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wamevaa fulana yeusi zenye maandishi yanayosomeka: “Kila unachofanya na kifanyike kwa upendo (Lets all that you do be done in love)”
Mwili wa Ulomi utasafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa maziko.
Miongoni mwa waombolezaji ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini (Turdaco) ambako Ulomi alikuwa akisoma fani ya sheria akiwa mwaka wa tatu.
Mwanachuo, Rahim Kalyango amesema alikuwa mtu aliyependa kujifunza na mwenye msaada, kwenye matatizo ya misiba alikuwa akitoa hadi gari kwa ajili ya usafiri.
“Chanzo cha kuwa maarufu chuoni wakati anakuja kuanza alikuwa anamiliki gari aina ya Coaster, ikitokea msiba kwa mwanafunzi alikuwa akilitoa. Hakuwa mbinafsi, alikuwa anapenda elimu ya sheria na ndoto yake siku moja awe mwanasheria,” amesema.
Kalyango amesema mara ya mwisho walikuwa naye Desemba 8, kwa ajili ya maandalizi ya mitihani na hata kwenye vipindi vya kawaida alikuwa anapenda kuchangia kwa kuwa alikuwa anakaa mbele.
“Tunachokikumbuka kwake ni ujasiri wa kumfikia mwalimu yeyote na kumweleza jambo analohitaji kujifunza, pia alikuwa mtu wa kusaidia, wakati mwingine alikuwa anatoa fedha kwa ajili ya ada,” amesema.
Amesema alikuwa msiri kiasi kwamba hakuwahi kuwaambia kuwa anajishughulisha na biashara za fedha kupitia mitandao ya simu.