Sababu Lwakatare kutojitoa kinyang’anyiro uenyekiti CUF

Dar es Salaam. “Endapo nikikuta jina la Profesa Ibrahim Lipumba katika karatasi za wagombea uenyekiti najitoa.” Hii ilikuwa kauli ya aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Lwakatare.

Licha ya kutoa kauli hiyo mara mbili kwa nyakati tofauti alipozungumza na Mwananchi, Lwakatare ameshindwa kuisimamia baada ya jana Jumatano, Desemba 18, 2024 kushiriki uchaguzi kuwania uenyekiti akichuana na Profesa Lipumba.

Mara ya kwanza Lwakatare alisema: “Nikikuta kuna fomu ya Profesa (Lipumba), mimi ya kwangu naiondoa… kwa sababu namheshimu sana na ameshanitamkia mara tatu kwamba hagombei, sasa tutakwendaje namna hiyo kwa kuviziana.”

Hata hivyo, Lwakatare ambaye ni mbunge wa zamani wa Bukoba Mjini ameliambia Mwananchi leo Alhamisi, Desemba 19, 2024 kuwa aliamua kutojitoa katika kinyanga’nyiro hicho baada ya wajumbe wanaomuunga mkono kumshawishi.

Katika uchaguzi ambao matokeo yalitangazwa usiku wa kuamkia leo, Lwakatare alishindwa kufua dafu mbele ya Profesa Lipumba aliyepata kura 216 kati ya kura 592 halali zilizopigwa. Lwakatare alipata kura 78.

Akisimulia namna ilivyokuwa ukumbini, Lwakatare amesema kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato alikuwa na kamati yake maalumu iliyokuwa ikimpa ushauri na kabla na baada ya kufika eneo la tukio walijadiliana kuhusu Profesa Lipumba na msimamo wake wa kutogombea.

“Tulijiuliza huyu jamaa (Profesa Lipumba), msimamo wake ni kutogombea, lakini mbona anakwepa kuzungumza na vyombo vya habari? Nikawaambia kuwa huyu jamaa nikiona jina lake sitaendelea na mchakato, nitajitoa,” Amesema na kuongeza:

“Jana kuna wajumbe kama 50 hivi walinisihi sana nisijitoe, nikawaambia nikikuta jina la Profesa sitagombea nitajitoa mbele ya mkutano mkuu. Tumefika ukumbini tukamuona Profesa ambaye katika hotuba yake ya ufunguzi akawaeleza wajumbe kutokana na presha ya watu… naachia demokrasia ifanye kazi yake na watu wafanye uamuzi wanavyoona,” amesema.

Kwa mujibu wa Lwakatare, kutokana na uzoefu wake katika siasa, alishaelewa maelezo ya Profesa Lipumba kwamba alikuwa akiigiza mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu, ikamlazimu kuwaita watu wake kujadiliana kwa mara nyingine.

“Nikawaambia mnaona hiyo ngoma, nikawaeleza kuwa huu ni mchezo ambao Profesa Lipumba ameucheza, lakini kuna mzee mmoja mwenye busara akaniambia kwa hatua tuliyofikia ukijitoa wale wajumbe wanaokuunga mkono wanaweza wakachukua hatua ya kukudhuru ni bora kuendelea.

“Akanishauri kuendelea na mchakato na nizungumze masuala yanayonihusu, kisha kunyamaza kimya. Kweli nilifanya hivyo, mwanzo mwisho, nikatoka nje. Tukiwa nje nikawaambia watu hii ngoma Profesa anashinda kwa sababu mimi ni mbobezi kwenye siasa na Lipumba anajua alichokifanya,” amesema.

Lwakatare aliyewahi kuwa mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa Chadema, amasema endepo angejitoa katika mchakato huo, wajumbe wangemwambia l kwamba walitaka kumpigia kura kwa wingi, lakini amejitoa.

Makamu mwenyekiti wa zamani wa CUF na mtalaamu wa masuala ya sheria, Profesa Abdallah Saffari amesema kabla ya mchakato alimweleza Lwakatare asigombee kwa sababu hawezi kushinda.

“Lwakatare ni rafiki yangu, nilimwambia achana na hii kitu, hautapata chochote hakunisikiliza, sasa amejitafutia kifo chake mwenyewe,” amesema alipozungumza na Mwananchi.

Related Posts