KIPA wa Kengold, Castor Mhagama ametuthibitishia hapa kijiweni ule usemi wa Mungu hakupi vyote au Mungu akikupa kilema, basi anakupa mwendo.
Jamaa anaonyesha kiwango kizuri sana anapokuwa uwanjani japo timu yake kiujumla inamuangusha kutokana na wachezaji wake wengine kushindwa kucheza vizuri katika mechi zao.
Unaweza usiamini ukihadithiwa ubora wa Mhagama ikiwa utaangalia msimamo wa ligi au matokeo ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata hadi kufanya iwe nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi.
Jamaa wamefungwa mabao 27 na ndio timu ambayo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi zaidi katika Ligi Kuu hadi sasa lakini kama umefuatilia kwa ukaribu mechi zao utaungana na sisi hapa kijiweni kuwa kipa wao hapaswi kulaumiwa.
Mhagama amekuwa akiokoa hatari nyingi ambazo zimekuwa zikielekezwa langoni mwa timu yake ambazo ukizihesabu zinazidi idadi ya mabao ambayo timu hiyo imefungwa kwenye Ligi Kuu.
Michomo mingi ambayo Mhagama amekuwa akiiokoa ni ile ambayo hata angekuwa akifungwa, ni vigumu kumlaumu lakini juhudi zake binafsi zinasaidia kuifanya Kengold isipate vipigo vya aibu hasa katika mechi kubwa.
Ukiangalia mwenendo wa Kengold kwenye Ligi Kuu msimu huu ulivyo, ni vigumu kuamini kama inaweza kukwepa janga la kushuka daraja kwa vile imekuwa na muendelezo wa kufanya vibaya na haionyeshi dalili za kuamka usingizini.
Labda pengine Mhagama ameshachungulia kesho ya Kengold kwenye Ligi Kuu akaona haitii matumaini hivyo ameamua kujipigania mwenyewe kwa kucheza vizuri ili azishawishi timu zimsajili baada ya msimu kumalizika.
Na kwa namna anavyocheza, kuna timu nyingi zitampelekea ofa mezani msimu ukimalizika na hili linatukumbusha kuwa fundi siku zote hawezi kulaĆa na njaa.