SIKU chache tu tangu Singida Black Stars kumalizana na mshambuliaji Joseph Guede kwa makubaliano ya pande mbili, uongozi wa klabu hiyo upo hatua za mwisho kumalizana na straika Mghana, Jonathan Sowah ili kuziba nafasi ya nyota huyo wa zamani wa Yanga mwenye uraia wa Ivory Coast.
Sowah anaungana na Mghana mwenzie, Frank Assinki anayecheza nafasi ya beki wa kati kukamilisha usajili wa timu hiyo dirisha hili la usajili ambalo walithibitisha kuboresha maeneo hayo mawili.
Chanzo cha kuaminika kutoka timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti, wachezaji hao wote wameshatua nchini kukamilisha taratibu za kujiunga na timu hiyo dirisha hili la usajili na wana imani wataongeza nguvu kwenye nafasi wanazocheza.
“Ni kweli tumemalizana na wachezaji hao ambao wamekuja kukamilisha idadi ya wachezaji 12 wa kigeni baada ya kuachana na Guede na kumtoa Mohamed Kamara ambaye ametimkia Pamba, hakutakuwa na ongezeko la mchezaji mwingine,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Maboresho yaliyofanywa yamezingatia ripoti ya walimu waliopo kutokana na mahitaji, ukiangalia eneo la ulinzi hatupo vizuri sana, tunaamini ujio wa Assinki utapunguza makosa madogo madogo yaliyopo huku eneo la ushambuliaji Elvis Lupia ameongezewa changamoto mpya.”
Kabla ya kutua Singida BS, iliwahi kuripotiwa Simba na Yanga zilijaribu kutupa ndoano zao kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita kuiwania saini ya Sowah wakati akiichezea Medeama ya Ghana, lakini akatimkia Libya kabla ya sasa kukubali kutua Tanzania kujiunga na Singida Black Stars.
Ndani ya Singida BS, mshambuliaji Elvis Rupia ndiye anayetegemewa zaidi kikosini hapo huku akiwa tayari ametupia mabao saba kati ya 20 yaliyofungwa na timu yake.
Singida Black Stars ipo nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 13, imeshinda nane, sare tatu na kufungwa michezo miwili wamefunga mabao 18 huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa.
Dirisha la usajili limefunguliwa Desemba 15, Singida Black Stars wao hadi sasa wametoa wachezaji wao wanne kwa mkopo, Israel Mwenda katua Yanga, Habib Kyomba Pamba, Najim Mussa ambaye amejiunga na Namungo FC na Kelvin Nashon aliyetimkia Pamba Jiji.