WINGA wa zamani wa Simba anayekipiga kwa sasa Geita Gold iliyopo Ligi ya Championship, Yusuph Mhilu amesema bado anatamani kucheza Ligi Kuu Bara na anafanya kila kitu kuhakikisha anaboresha kiwango chake na kushawishi timu mbalimbali kumrejesha kwenye michuano hiyo.
Mhilu alishuka Geita msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara na hadi sasa akiwa na timu hiyo inayoshika nafasi ya pili katika Ligi ya Championship amefunga bao moja tu katika mechi 12 ilizocheza timu hiyo.
Winga huyo aliyewahi kutamba Ligi Kuu akiwa na Kagera Sugar alisema Championship itamsaidia kurejesha ubora wake na kumuweka sokoni ili awe kivutio tena kwa tikubwa kama alivyowahi kukipiga akiwa na miamba ya soka nchini Simba na Yanga.
“Binafsi nimejiwekea malengo mengi hii Ligi (Championship) ndiyo naicheza kwa mara ya kwanza na nimekubali kuwepo ili kucheza mechi nyingi na kurudisha kiwango changu. Unapocheza mara nyingi unaendelea kuimarika na nashukuru kuwa Napata nafasi ya kucheza,” alisema Mhilu.
Alisema licha ya kutofunga mabao mara kwa mara lakini anapambana kuhakikisha anatoa msaada kwa timu yake kufikia malengo kwa kutoa pasi za mabao na kufunga anapopata nafasi kwani ndivyo vinatumika kumtangaza sokoni mchezaji.
“Soka letu kwa sasa wanaangalia takwimu namna ulivyoshiriki kwenye mafanikio ya timu yako, kwa hiyo najitahidi kufunga na kuasisti kwa kuwa soka letu ukifunga ndiyo unatangazika na soka lako linakuwa zuri,” alisema Mhilu.
Katika Ligi ya Championship, Geita Gold inakamata nafasi ya pili ikiwa na alama 27 baada ya michezo 12 ikiwa imeshinda nane, sare tatu na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 18 na kuruhusu sita. Mtibwa Sugar inaongoza ikiwa na alama 29.