DKT. KIRUSWA ASISITIZA MRADI WA KUDU GRAPHITE KUANZA KWA WAKATI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesisitiza kuanza kwa wakati kwa Mradi wa Uchimbaji Madini ya graphite (kinywe) na kwa mujibu wa Matakwa ya Sheria ya Madini alipokutana na Mwenyekiti Mpya wa Kampuni ya Evolution Energy Minerals, katika kikao kilicholenga kufahamiana na kujadili maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kupitia kampuni ya KUDU Graphite.

Kampuni ya Evolution Energy Minerals ni mbia na Serikali yenye umiliki wa hisa za asilimia16 zisizohamishika kwenye kampuni ya ubia ya KUDU GRAPHITE inayomiliki mradi wa uchimbaji madini hayo eneo la Chilalo, Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.

Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara leo Desemba 19, jijini Dar Es Salaam ambapo Dkt. Kiruswa ameeleza kwamba, matamanio ya Serikali ni kuona miradi ya kimkakati iliyopewa leseni za uchimbaji madini inaanza kwa wakati.

β€˜β€™Mhe. Rais, ameboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hivyo wawekezaji mnapopata fursa ya kuaminiwa na Serikali na kupewa leseni za uchimbaji madini kuhakikisha uwekezaji unafanyika ipasavyo kwa mujibu wa makubaliano na Sheria zetu za nchi ili kuleta maendeleo kwa jamii zinazozunguka miradi hiyo na Taifa kwa ujumla,’’ amesisitiza Dkt. Kiruswa.

Aidha, Dkt. Kiruswa amewataka viongozi wa kampuni hiyo kuwa na ratiba ya utekelezaji wa mradi kwa kila hatua na kumwagiza balozi wa mradi huo kutoka Wizara ya Madini Mhandisi Neema Mwafumbira kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu uendelezaji wa mradi huo kwa mujibu wa mpango wa uendelezaji mradi huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kampuni ya Evolution Energy Minerals Bw. Robin Birchall amemhakikishia Dkt. Kiruswa kuwa kampuni hiyo itafuatilia kwa karibu utekelezaji wake ili mradi huo uanze haraka iwezekanavyo na kuleta mafanikio yanayotarajiwa na taifa kupitia rasilimali madini.

Vilevile, Bw. Birchall amesema, mradi huo umechelewa kuanza kutokana na mapungufu ya usimamizi uliokuwepo kwa viongozi wa juu, hivyo kampuni hiyo imefanya mabadiliko makubwa kwa kuteua Mkurugenzi Mkuu Mtendaji, Mkurugenzi Mkuu wa Fedha na Mwenyekiti mpya.

Pia, amemhakikishia Dkt. Kiruswa kuwa, uongozi wake utahakikisha kampuni hiyo inawaendeleza watanzania kwenye kada muhimu na zenye upungufu wa wataalam akitolea mfano wataalam wa kukadiria mashapo ya madini wanaotambulika kimataifa.

Wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dar Es Salaam Gabote Masanja, Meneja Mkazi wa kampuni ya KUDU GRAPHITE Dkt. Heavenlight Kavishe na balozi wa mradi huo kutoka Wizara ya Madini, mhandisi Neema Mwafumbira.

*#InvestInTanzaniaMiningSector*

*#ValueAdditionforSocio-EconomicDevelopment*

*#UongezajithamaniMadinikwaMaendeleoyakijamiinakiuchumi*

*#Vision2030: MadininiMaishanaUtajiri*

*#MadiniDiary*

Related Posts