TULISIKIA na kuyasoma mengi kuhusu winga Ellie Mpanzu hasa kuhusu sifa zake pindi awapo uwanjani wakati huo akiichezea AS Vita Club ya DR Congo hasa uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao.
Na sifa hizo zikafanya timu zetu hapa Tanzania kushawishika kumsajili zikiamini kwamba ataongeza kitu na wakawa ni Simba ambao walifanikiwa kupata saini yake.
Katika hiki kijiwe tuna kumbukumbu ya Simba kumsajili Mpanzu nje ya kipindi cha dirisha la usajili katika kinachoonekana kutokuwa kwao tayari kuona mchezaji huyo ananaswa na timu nyingine hapo baadaye na wao kuzidiwa kete.
Hatimaye subira imevuta heri, dirisha la usajili limefika na jina la Ellie Mpanzu limeingia katika orodha ya wachezaji watakaoitumikia Simba msimu huu hivyo muda mfupi ujao tutamuona uwanjani.
Ule muda wa kuthibitisha kauli ya kuona ni kuamini umefika ambapo sasa wenyewe tutajionea kama Mpanzu ni chuma kweli na atakuwa usajili bora zaidi kwa Simba au la na sio kuendelea kusikia au kusoma tu sifa zake.
Kile ambacho alikifanya huko AS Vita Club na kwenye mazoezi au mechi za kirafiki za kimyakimya za Simba huu ndio muda wa Mpanzu kutuonyesha katika mechi za kibabe za Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.
Akishindwa kuonyesha ajiandae na mashambulizi ambayo ataelekezewa kwani watu tayari wameshapewa matarajio makubwa kuhusu yeye na wameaminishwa kuwa ni nyota wa daraja la juu.
Na kama akifanikiwa, hapana shaka atakuwa miongoni mwa wafalme wa Simba na Ligi yetu kiujumla maana Watanzania huwa hawana hiyana katika kumjaza sifa hata na zile asizostahili mchezaji anayefanya vizuri.
Ni yeye mwenyewe Mpanzu wa kuamua kuondoka na kijiji cha wabongo kwa kupiga soka la kibabe au kujikwamisha kwa kuonyesha kiwango cha kawaida.