Kifo cha hakimu chasogeza mbele kesi ya Boni Yai, Malisa

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Januari 15, 2025 kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha umma, inayomkabili meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai.

Mshtakiwa mwingine ni katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024 ni Godlisten Malisa, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Jacob, mkazi wa Mbezi Msakuzi na Malisa wanakabiliwa na mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yamkabili Jacob pekee.

Kesi ilipangwa kuanza kusikilizwa leo Alhamisi, Desemba 19, 2024 lakini imeshindikana kutokana na kifo cha Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Maximillian Malewa, aliyefariki dunia Desemba 17, 2024.

Wakili wa Serikali, Asiat Mzamiru ameeleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo kuwa kesi imeitwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji na upande wa mashtaka tayari una shahidi mmoja.

“Upande wa mashtaka tuna shahidi mmoja ambaye amekuja kwa ajili ya kutoa ushahidi na yupo ndani ya Mahakama yako,” ameeleza.

Hakimu Swallo amesema kwa kuwa kuna msiba wa hakimu mwezao na wanajiandaa kwenda msibani, hawataweza kuendelea na usikizwaji wa shauri hilo, hivyo kuiahirisha hadi Januari 15, 2025 itakapoanza kusikilizwa. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Washtakiwa wanashtakiwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jacob anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kinyume cha kifungu cha 16 cha sheria hiyo.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupotosha umma. Anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani twitter) wenye jina la Boniface Jocob@ExMayor Ubungo.

Shtaka la pili anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii Machi 19, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mtandao wake akihusisha polisi na mauaji ya dereva wa magari ya watalii.

Shtaka la tatu la kutoa taarifa za uongo linamkabili Malisa anayedaiwa kulitenda Aprili 22, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anadaiwa kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram wenye jina la Malisa_gj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka “Tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi Aprili 2024.”

Kwa mara ya kwanza Jacob na Malisa walifikishwa mahakamani hapo Mei 6, 2024 kujibu mashtaka hayo.

Taarifa ya msiba iliyotolewa na kusainiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Frank Kiswaga imeeleza Malewa aliyekuwa pia Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, alifariki dunia jioni ya Desemba 17, 2024.

Malewa amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mloganzila.

Taarifa hiyo imeeleza taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake, Misugusugu, wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Imeelezwa mazishi yatafanyika Jumamosi Desemba 21, katika Kijiji cha Kilacha, Himo mkoani Kilimanjaro.

Related Posts