Hivi ndivyo unavyoweza kuomba ulinzi binafsi wa Polisi

Dar es Salaam. Kufuatia madai ya kutishiwa uhai wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, baadhi ya wanasheria wametoa mwongozo wa kuomba ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa mtu binafsi mwenye tishio kama hilo.

Lissu alitoa taarifa kupitia ukurasa wake wa X Desemba 16, akidai kuwepo watu wanaolenga kumshambulia na sasa ameanza kuvaa vazi la kujikinga na risasi akihofia usalama wake.  

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari Desemba 17, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliyafananisha madai ya Lissu na uhuru wake wa maoni, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha raia wote wanakuwa salama pamoja na mali zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 18, baada ya kurudisha fomu yake ya kugombea uenyekiti wa Chadema, Lissu akiwa amevaa vazi la kujikinga na risasi (bullet proof) alisema hajafurahishwa na kauli ya Jeshi la Polisi, na ndio maana ameanza kujilinda mwenyewe.

Lissu aliyewahi kushambuliwa na risasi 16 na watu wasiojulikana akiwa mjini Dodoma Septemba 7, 2017, aliwahi kutoa taarifa kwa waandishi wa habari kuwa kuna magari yanayomfuatilia siku chache kabla ya shambulio hilo.

Akizungumzia utaratibu wa mtu binafsi kupewa ulinzi wa polisi endapo anapata changamoto hiyo ya kutishiwa maisha yake leo Desemba 19, mwanasheria maarufu John Seka amesema kwa ujumla Polisi wana wajibu kisheria kulinda raia na mali zao.

“Kimsingi mtu anapaswa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi ya kuwepo tishio la usalama wake, halafu wao watachunguza kisha watatoa ulinzi, ikiwa pamoja na kumpa namba atakayokuwa akipiga muda wowote anapoona kuna tishio, au watamshauri aongeze ulinzi binafsi au wanaweza kuleta gari la doria mahali anapoishi,” amesema Seka.

Maoni hayo yameungwa mkono na mwanasheria Mwingine aliyeomba asitajwe jina lake kwa sababu za kibiashara, akisema sheria inaelekeza polisi kulinda raia na mali zao kwa usawa.

“Kwa ujumla sheria inaelekeza polisi kulinda raia na mali zao na pia inaelekeza kutoa ulinzi kwa viongozi. Sasa ikitokea kuna mahitaji maalumu, mtu anapaswa kwenda kutoa taarifa polisi, ambao watafungua jalada la uchunguzi kwa sababu hiyo ni jinai.

Amesema wakishafanya uchunguzi wao na ujiridhisha, watatoa ulinzi kwa mtu huyo.

Hata hivyo, amesema hakuna kifungu cha sheria kinachotoa mwongozo huo, isipokuwa litachukuliwa kuwa ni tukio la kijinai.

Alipoulizwa kuhusu njia za kutoa taarifa polisi, mwanasheria huyo nguli amesema, “mtu anaweza kwenda kuripoti polisi au hata kutoa taarifa hadharani kwenye vuyombo vya habari.”

Related Posts