Bukoba. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewaomba wafanyabiashara kutambua fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Kagera na kuzichangamkia ili kukuza uchumi wa mkoa huo.
Akizungumza wakati wa kufungua Kongamono la wafanyabishara katika tamasha la Ijuka Omuka leo Desemba 19, 2024 Dk Biteko amesema anatamani kuona wawekezaji wanazichangamkia fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Kagera.
Amesema ralisimali zilipo mkoani humo ikiwemo ardhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji, hali nzuri ya hewa ni nyezo muhimu zinazoweza kuvutia uwekezaji utakaozalisha ajira.
“Ni wakati wa wawekezaji wakubwa sasa kuuona mkoa kagera kama sehemu sahihi sasa ya kuwekeza miradi mbali mbali kama viwanda mahotel makubwa maana mkoa umesheni vivutio vya utarii na maeneo mazuri ya kuwekeza,” amesema Dk Biteko.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amemuomba Dk Biteko kuwezesha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Omkajungati uliopo wilayani Misenyi.
Aidha Bashungwa ameongeza kuwa Tamasha la Ijuka Omuka Festival la mwaka jana kipindi yeye ni mgeni rasmi linaonekana kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi hivyo anatamani kuona maendeleo yanaendana na historia ya mkoa ya kuwa na wasomi wengi.
“Kipindi nikiwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Ijuka Omuka liliotukutanisha mwaka jana kama hivi kuna mikakati mingi iliwekwa na sasa imeanza kuzaa matunda makubwa ya kimaendeleo hivyo kupitia uwekezaji basi tuweze kwendana na historia yetu ya kimkoa kuwa na wasomi wengi,” amsema Bashungwa.
Awali, akiwasilisha taarifa ya mkoa huo Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa amesema mkoa huo una idadi ya watu wanaishi 2.9 milioni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 huku akitaja pato la mkoa huo kuwa Sh4.3 trilioni na pato la mkazi mmoja mmoja likiwa ni milioni 1.4 kwa mwaka.