Morogoro. Mwili mmoja wa marehemu wa ajali ya Coaster umetambuliwa na hivyo kufanya jumla ya miili 11 ya waliokufa katika ajali hiyo kutambuliwa huku miili minne ikiwa bado haijatambuliwa.
Akizungumza na Mwananchi mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu amemtaja marehemu aliyetambuliwa leo kuwa ni Sauda Sozigwa (35).
Dk Nkungu amesema kuwa kati ya miili hiyo 11 iliyotambuliwa saba ya wanaume na minne ya wanawake.
“Baada ya kutambuliwa tayari miili 9 ilishachukuliwa na ndugu kwa ajili ya kwenda kuzika na miili miwili bado imehifadhiwa wakati ndugu wakiendelea na mipango ya mazishi na nadhani kesho wanaweza kuja kuchukua miili ya wapendwa wao,” amesema Dk Nkungu.
Kuhusu majeruhi Dk Nkungu amesema hospitalini hapo wamebaki wanne baada ya majeruhi wawili kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI) kwa ajili ya vipimo na matibabu ya kibingwa huku majeruhi mmoja akiruhusiwa kutoka hospitali hapo.