Dar es Salaam. Kampuni ya SmartLab kwa kushirikiana na shirika la ubunifu wa hali ya hewa barani Ulaya EIT Climate-KIC, wamezindua mpango wa kukabiliana na kustahilimi mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania.
Mkurugenzi wa biashara wa Smart Lab ambayo ni kampuni tanzu ya Smart Africa Group, Larry Ayo amesema ubunifu huo unakabiliana na changamoto muhimu za mabadiliko ya hali ya hewa huku ukiinua maisha ya jamii zinazohitaji msaada zaidi.
Ayo ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 19, 2024 katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Programu ya Adaptation and Resilience -ClimAccelerator jijini Dar es Salaam.
“Mpango huu ulipokea maombi ya wajasiriamali zaidi ya 170 kutoka mikoa ya Iringa, Arusha, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Singida. Baada ya mchujo, wajasiriamali 10 walichaguliwa, wakiwemo, Tanzania Viable Farms, Herveg.05, Ndugunamiti Enterprises Ltd, Kilimomax Solutions, insectUp, Rada 360 Limited, Thorntsorn, Kesho Technologies Company Limited, DMA, na Addrone Digital,” amesema .
Amesema kupitia programu hiyo wajasiriamali hao watapata ushauri maalumu, rasilimali na mtandao wa ushirikiano ili kuongeza athari zao na kuunda suluhisho endelevu kwa jamii za vijijini na mijini.
Mpango huo unaojulikana kama ‘Adaptation and Resilience ClimAccelerator’ unalenga kukuza suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania ukihusisha wabunifu na wagunduzi katika eneo la mabadiliko ya tabia nchi.
Mpango huu unaotumia mifumo kusaidia miji, mikoa, nchi na viwanda kufikia malengo ya hali ya hewa umeshatekelezwa katika mataifa mbalimbali.
Meneja Mkuu wa Programu ya Global Resilience Partnership, Gerald David alisema programu hiyo inaonesha nguvu ya ushirikiano katika kushughulikia athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
“Programu kama hizi zinasaidia wabunifu wa ndani ya nchi kukabiliana na changamoto za kimataifa. Uzinduzi wa leo unaonyesha dhamira za dhati za washirika wote walioshiriki. Tunawashukuru EIT Climate-KIC na Irish Aid kwa kutuamini na kutuunga mkono tunapojenga mustakabali endelevu kwa Tanzania,”amesema David.
Tangu 2019, EIT Climate-KIC imesaidia zaidi ya wabunifu 300 wa Kitanzania kupitia programu mbalimbali.
Awamu inayofuata ya mpango huu itaanza mapema 2025, ikilenga kusaidia wajasiriamali waliochaguliwa kukabiliana na changamoto za hali ya hewa na kuimarisha uthabiti katika jamii za vijijini.
Mkurugenzi wa Biashara wa SmartLab, Larry Ayo akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Programu ya Adaptation and Resilience -ClimAccelerator jijini Dar es Salaam.