DC Mpogolo awataka wenyeviti wa mitaa kujenga umoja, mshikamano

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Ilala wametakiwa kujenga umoja na mshikamano kwa sababu wanategemewa na wananchi kwa kuwa ndio kimbilio.

Wito huo umetolewa Desemba 18,2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati akifunga semina elekezi kwa wenyeviti hao waliochaguliwa hivi karibuni.

Amesema eneo pekee ambalo mwenyekiti anaweza kuonyesha uwezo wake ni namna anavyoweza kujenga umoja na mshikamano kwenye mtaa wake na kwamba mwenyekiti anavyokubalika anaifanya Serikali ikubalike.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Ilala, Seif Mwera, akizungumza wakati wa semina elekezi kwa wenyeviti waliochaguliwa hivi karibuni.

“Sisi ni watumishi wa umma tumeomba kura kwa ajili ya kwenda kuwatumikia watu hivyo, hakuna shida yoyote ya watu ambayo mwenyekiti atasema haimuhusu, shida za watu katika mitaa yetu zinatuhusu kwahiyo tunasisitiza mkae karibu na watu ili kwa pamoja tuweze kushiriki kutatua shida zao,” amesema Mpogolo.

Amesema mafunzo hayo yalikuwa na tija kwa sababu zaidi ya nusu ya wenyeviti waliochaguliwa ni wapya hivyo walihitaji kupewa mafunzo namna gani wanaweza kufanya kazi zao na kuwakumbusha pia wale wa zamani wajue wajibu wao kwenye usimamizi.

“Wamekumbushwa namna ya ujenzi wa mahusiano na muundo wa serikali za mitaa unavyofanya kazi zake, ni semina ambayo imekuwa nzuri. Ni wajibu wao kwenda kusimamia masuala ya ulinzi na usalama kwenye mitaa yao, kuhakikisha halmashauri inakusanya mapato yake yanayostahili na kusimamia miradi kwa sababu miradi yote inayotekelezwa iko kwenye mitaa yao,” amesema.

Mkuu huyo wa wilaya pia amesisitiza suala la michango shuleni kamati za shule zishirikiane na wazazi kupanga kiasi cha kuchangia lakini michango mingine ni mpaka wapate kibali.

Mmoja wa washiriki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kidole uliopo Kata ya Msongola, Amos Chacha, amesema atazingatia mafunzo aliyoyapata kuhakikisha mtaa huo unakuwa na amani na kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.

“Tunashukuru sana ofisi ya mkuu wa wilaya na mkoa kwa kuona ni vyema kabla hatujaingia kwenye majukumu yetu tupate semina elekezi, ni semina ambayo kwa mwaka huu imekuwa tofauti, imetufungua kwa ajili ya utendaji kazi na majukumu ya wenyeviti wa serikali za mitaa. Kwa namna ambavyo tumejifunza nimetambua mambo mengi ya msingi ambayo natakiwa nikayasimamie na kuyatekeleza,” amesema Chacha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti Wilaya ya Ilala, Seif Mwera, amesema wenyeviti wanaokosea sheria ifuate mkondo wake na kuahidi kuwa hawatarudia makosa yaliyopita.

Watoa mada katika mafunzo hayo walikuwa wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.

Related Posts