RC Babu ataka waliopo maeneo hatarishi mkoani Kilimanjaro kuondoka mara moja

Moshi. Kufuatia mvua zinazonyesha maeneo mbalimbali Mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu amewataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi katika mkoa huo kuondoka mara moja ili kuepuka majanga ya hatari yanayoweza kujitokeza.

Babu ametoa maelekezo hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC), kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, uliopo Manispaa ya Moshi.

Amesema mvua zinazonyesha zimeleta athari kubwa katika baadhi ya Wilaya za mkoa, hususani Wilaya ya Mwanga na Same, ambapo baadhi ya nyumba zimeathiriwa.

“Niwatake na kuhakikisha wananchi walioko kwenye maeneo hatarishi wanatoka katika maeneo hayo hasa nyakati hizi za mvua,” amesema Babu.

Ameongeza kuwa mvua za vuli zimeharibu nyumba na vifaa, ingawa alifafanua kuwa, kwa bahati nzuri, Wilaya ya Same hakukuwa na vifo, lakini Wilaya ya Mwanga amefariki mtoto wa darasa la tatu.

Aidha, Babu ametoa tahadhari kuhusu mvua hizo akisema, “Tunaipenda mvua, lakini zimekuja kwa kasi na kuleta athari. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha usalama wa wananchi, hasa wale wanaoishi kwenye maeneo hatarishi.”

Pamoja na mambo mengine, amezitaka mamlaka husika kuhakikisha mikakati ya kuzibua mifereji na madaraja yaliyojaa tope inashughulikiwa ili kuruhusu maji kupita kwa mwelekeo wake.

“Nizielekeze mamlaka zinazohusika na barabara kuhakikisha barabara zinakarabatiwa na zinapitika, hasa kipindi hiki cha mvua, ili huduma za usafiri na usafirishaji ziendelee kuwa na uhakika,” amesema Babu.

Baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, katika Kata ya Mji mpya, walielezea changamoto zao na kuomba serikali kuangalia namna ya kuwatafutia maeneo mengine mbadala, kwani wengi hawana pakwenda.

Mkazi wa Kwakomba, Hadija Juma  ameiomba serikali kuwatafutia maeneo mengine kwa kuwa familia zao zinahatarishwa na mafuriko na hawana pakwenda.

 “Tupo kwenye maeneo hatarishi na mwaka huu maeneo yetu yalipatwa na mafuriko, na baadhi ya nyumba zilisombwa na maji na watu kupoteza maisha, Serikali itusaidie, maana hatuna pakwenda,” amesema Hadija.

Elinihaki Mbwambo, mkazi wa Kahe, alikubaliana na tamko la Mkuu wa Mkoa, akisema kuwa waliopo ndani ya mita 60 kutoka mto wanapaswa kuondoka, huku akisisitiza umuhimu wa serikali kuwafidia wananchi hao na kuwapa maeneo mengine.

 “Serikali iangalie namna ya kutusaidia kwani hali ngumu ya maisha inafanya watu hawawezi kujisaidia na kujenga makazi mapya,” amesema.

Related Posts