Dodoma. Mahakama Kuu, imeamuru kurudishwa kazini kwa aliyekuwa polisi mkoa wa kipolisi wa Tarime Rorya, WP 8608, Koplo Ester Mdeme, aliyefukuzwa kazi 2023 baada ya mifuko mitatu ya mchanga wenye dhahabu kutoweka.
Uamuzi huo umetolewa Desemba 17, 2024 na Jaji Abdi Kagomba, kufuatilia maombi ya mapitio ya mahakama, kupinga kufukuzwa kazi yaliyofunguliwa na Mdeme dhidi ya Kamanda wa Polisi Tarime na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).
Katika maombi hayo yanayofahamika, Polisi huyo wa zamani alimuunganisha pia Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kama mjibu maombi wa tatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa nne.
Kiini cha kufukuzwa ni kuwa Mdeme alikuwa ni askari aliyekuwa akihudumu katika kituo cha Nyamwanga katika mkoa wa kipolisi wa Tarime Rorya hadi alipofutwa kazi Januari 23, 2023 aliposhitakiwa na kuhukumiwa kijeshi.
Ilidaiwa Januari 10, 2023, askari huyo alikwenda doria yeye na askari wenzake kwa ajili ya kufuatilia wananchi waliokuwa wamevamia Mgodi wa North Mara kwa lengo la kuiba mchanga ulikuwa unadhaniwa kuwa na madini ya dhahabu.
Katika operesheni hiyo, mleta maombi na askari wenzake inadaiwa walifanikiwa kukamata mifuko mitano maarufu kama ‘Bob Marley Bags’ yenye madini kutoka kwa wavamizi lakini walipoulizwa, walikabidhi mifuko miwili tu getini.
Picha katika kamera za usalama (CCTV) zilipoangaliwa, zilionyesha kuwa timu hiyo ya polisi ilikuwa imekamata mifuko mitano hivyo timu hiyo iliyokuwa katika gari la doria LV 45 walikamata na kushitakiwa kwa utovu wa nidhamu.
Wakashitakiwa katika mahakama ya kijeshi na kutiwa hatiani na kufukuzwa kazi akiwamo Mdeme na hata alipokata rufaa kwa IGP ambayo ndio mamlaka ya mwisho ya rufaa kwa cheo chake, lakini jitihada zake hizo ziligonga mwamba.
Hakuridhika na akabisha hodi katika milango ya mahakama ili kupata kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review) na kufanikiwa kupata, akafungua maombi akitaka uamuzi wa kumfuta kazi ubatilishwe.
Pia katika maombi hayo, akaiomba mahakama itoe amri kwa IGP ambaye ni mjibu maombi wa pili, kumrejesha kazini, akitoa sababu mbalimbali ikiwamo ukiukwaji wa sheria na taratibu zinazosimamiwa mashitaka dhidi ya polisi.
Hoja za kisheria zilivyokuwa
Kupitia kwa jopo la mawakili wake watatu ambao ni Charles Simon, Grace Benny na Irene Ishengoma, walidai uamuzi wa kumfuta kazi ulikiuka kanuni za uendeshaji Jeshi la Polisi (PGO) kuhusiana na uandaaji wa hati ya mashitaka.
Akiwasilisha hoja kwa niaba ya mawakili wenzake, Wakili Simon alieleza kifungu hicho kinataka kabla ya kuandaa hati ya mashitaka dhidi ya polisi mtuhumiwa, lazima kuwepo uchunguzi wa awali kama tuhuma ni za kweli ama la.
Halikadhalika alisema PGO namba 106(6) haikuzingatiwa licha ya kuweka sharti la lazima kuwa kumbukumbu za mwenendo wa shauri la kinidhamu lazima liwe na sehemu mbili, yaani uchunguzi wa awali na ushahidi uliochukuliwa.
Pia uamuzi wa kumfuta kazi ulikiuka taratibu kwa kuwa unataka ofisa anayeshughulikia shauri la nidhamu ni lazima azingatie kuwa hapakuwa na shahidi yeyote aliyethibitisha kumuona muombaji akichukua mifuko hiyo.
Halikadhalika wakili huyo alisema mahakama ya kijeshi haikuzingatia utetezi wa mteja wao, alieyeeleza kuwa hakuwahi kwenda katika eneo ambalo mifuko hiyo ilikamatwa wala kuiona mifuko hiyo na timu hiyo ilikuwa na kiongozi wake.
Hoja ya nne ilikuwa ni hitimisho la nidhamu halikuwa na maana na hakuna mamlaka yoyote yenye busara ingeweza kufikia uamuzi kama huo lakini pia ilikiuka haki ya asili kwa kumweka mahabusu zaidi ya saa 24.
Wakili huyo alisema PGO namba 106 aya ya 55, inazuia Ofisa wa Polisi kuwekwa mahabusu kwa zaidi ya saa 24 pale anaposhitakiwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu lakini yeye aliweka mahabusu kati ya Januari 16 hadi 27.
Akijibu hoja kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na dosari, wakili wa Serikali, Nicodemus Agweyo, aliirejesha mahakama katika hati ya kiapo cha nyongeza cha wajibu maombi kikionyesha iliandaliwa na kusainiwa na ASP Mnacco.
Kuhusu hoja kuwa ushahidi uliotolewa haukuwa umemuunganisha Mdeme moja kwa moja na tuhuma hizo, wakili Agweyo alisema katika maombi ya mapitio, mahakama haiombwi kuchambua kuchambua upya ushahidi.
Wakili huyo alisema hilo lingeweza kufanyika katika hatua ya rufaa na kuongeza kuwa kuna msimamo wa mahaka juu ya suala hilo akisema mapitio ya mahakama yanahusu kanuni na mchakato uliosababisha uamuzi unaopingwa.
Kuhusu uchunguzi wa awali kama ulifanyika kabla ya kuandaa mashitaka, wakili Agweyo hakukubaliana na hoja hiyo akisema uchunguzi huo ulifanyika na ndio maana sio maofisa wote walikuwepo katika operesheni hiyo walishitakiwa.
Halikadhalika kuhusu muombaji kunyimwa haki ya kusikilizwa kutokana na kuwekwa mahabusu kwa siku 12, wakili huyo aliirejesha mahakama katika aya ya tano ya hati ya kiapo kwamba baada ya upelelezi kukamilika waliachiwa.
Baada ya kukamilika kwa hoja hizo, Jaji alisema hoja zinazopaswa kuamuliwa ni mbili ambazo ni kama mchakato mzima wa shauri la nidhamu na kumfuta kazi muombaji na rufaa yake iliyokataliwa, ulikiuka haki ya asili na sheria za nchi.
Hoja ya pili kwa mujibu wa Jaji, ni kama maombi hayo ya mapitio ya kupinga kufutwa kazi ya muombaji yana mashiko ama la ili sasa mahakama itumie mamlaka ya kisheria iliyonayo na kutoa amri zinazoombwa na muombaji.
Jaji alisema kulingana na kiapo cha muombaji na mawasilisho ya mawakili wake, ni kuwa muombaji anapinga uamuzi wa kumfuta kazi ndani ya Jeshi la Polisi akisema uligubikwa na ukiukwaji wa taratibu na maamuzi.
Kulingana na muombaji, PGO inataka kuwepo kwa uchunguzi wa awali kabla ya kuandaa hati ya mashitaka lakini muombaji anaeleza kuwa hilo halikufanyika.
Jaji alisema amepitia uamuzi huo wa RPC Tarime na IGP na viapo lakini hakuona uthibitisho wowote kuwa uchunguzi huo wa awali ulifanyika na hata waliporuhusiwa kuongeza kiapo, bado hawakuwasilisha uthibitisho huo.
“Kwa vile kuna hisia kutoka kwa muombaji kuwa uchunguzi huo haukufanyika na wajibu maombi wanasema ulifanyika, basi lilikuwa ni jukumu la wajibu maombi kuwasilisha ushahidi wa maandishi kuthibitisha hoja hiyo,” alisema.
Jaji alisema kifungu cha 112 cha sheria ya ushahidi kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, wajibu wa kuthibitisha shitaka ni wa washitaki jambo ambalo katika mwenendo wa shauri hilo la mahakama ya Polisi halioni.
Mbali na hilo, Jaji alisema katika kiapo cha nyongeza, wajibu maombi walieleza kuwa hati ya mashitaka ilisainiwa na ASP Mnacco Januari 13, 2023 lakini baada ya kupitia kwa umakini hati ya mashitaka haoni mahali iliposainiwa.
“Kwa sababu hiyo, nakubaliana na wakili wa mjibu maombi kwamba hati ya mashitaka ilikuwa mbaya kisheria na mimi nakubaliana naye na natamka uamuzi wa kumfuta muombaji kazi ulikuwa ni mbaya kisheria,” alisema Jaji.
Alisema baada ya kupitia mawasilisho ya mawakili, ana maoni kuwa operesheni zozote za polisi ziwe za chini kwa chini zinapaswa kuthaminiwa, lakini katika shauri hilo namna polisi walivyotendewa inaacha maswali.
Alisema ameridhika kulikuwa na ukiukwaji wa sheria katika taratibu na uamuzi wa kumfuta kazi polisi huyo hivyo uamuzi wa kumfuta kazi unabatilishwa na mahakama hiyo inamwamuru IGP kumrejesha kazini muombaji huyo.