Rais Samia kuongoza Maadhimisho ya Miaka 25 ya TAWJA Arusha

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), yatakayofanyika kwa siku tano kuanzia Januari 19 hadi 23, 2025, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Arusha.

Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa Rufani Barke Sehel, alithibitisha hayo leo Desemba 19, 2024, jijini Dar es Salaam, akisema maadhimisho hayo yatatoa fursa ya kujadili masuala ya haki na usawa wa kijinsia.

“Tutaangazia changamoto zinazotokana na ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti, na nini kifanyike kukabiliana nazo,” amesema Jaji Sehel.

Jaji mstaafu Sophia Wambura, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi, amesema TAWJA imepata mafanikio makubwa katika miaka 25, yakiwemo kuimarisha usawa wa kijinsia katika Mahakama na jamii.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aisha Bade, ameongeza kuwa elimu kuhusu dhamana itatolewa kutokana na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wake.

Maadhimisho hayo yatashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo UN Women, UNDP, na UNICEF.

Related Posts